
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesogeza mbele tarehe ya kikao cha uteuzi wa wagombea wa nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani kupitia chama hicho hadi Julai 28, 2025. Awali, kikao hicho kilipangwa kufanyika Julai 19 na 20 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 19,2025 jijini Dodoma, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Ndg. Amos Makalla, amesema kikao hicho kitatanguliwa na vikao vingine muhimu vya chama, ikiwemo Kikao cha Kamati Kuu ya CCM na Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) vinavyotarajiwa kufanyika Julai 26, 2025.
“Niwatake wagombea wote kuwa watulivu wakati huu wa kusubiri uteuzi. Chama chetu kimejidhatiti kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mmoja. Tunapitia kwa makini wasifu (CV) za wagombea wote ili kupata viongozi makini,” alisema Makalla.
Ameongeza kuwa mwaka huu kumekuwa na mwitikio mkubwa wa watia nia, ambapo kwa nafasi ya Ubunge na Uwakilishi, zaidi ya watu 10,000 wamejitokeza, huku nafasi ya Udiwani ikivutia zaidi ya watia nia 27,000.
"Kwa idadi hii kubwa, ni wazi kuwa watu wamehamasika sana. Tunachokitaka kama chama ni kuhakikisha kila mmoja anatendewa haki,” alisisitiza Makalla.
No comments:
Post a Comment