WAZIRI MKUU AHIMIZA MALEZI YA KIMAADILI NA USHIRIKIANO WA KIJAMII - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, May 24, 2026

WAZIRI MKUU AHIMIZA MALEZI YA KIMAADILI NA USHIRIKIANO WA KIJAMII


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema jamii inapaswa kurejea katika misingi ya malezi ya pamoja na uwajibikaji wa kijamii ili kujenga kizazi chenye maadili, kinachoheshimu viongozi, wazazi pamoja na taasisi za jamii.

“Tunataka kujenga jamii inayoguswa na changamoto za wengine. Maadili mema yanaanzia kwenye malezi ya familia na jamii kwa ujumla,” amesema Dkt. Mwigulu.

Dkt. Mwigulu amesema hayo leo Jumapili, Mei 24, 2026 aliposhiriki Ibada ya Pentekoste katika Kanisa Kuu la KKKT Usharika wa Iringa Mjini iliyoongozwa na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Dkt. Blaston Gavile.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini katika kuimarisha huduma za kijamii, malezi ya maadili na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi.

“Ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini ni jambo kubwa sana katika maendeleo ya nchi yetu. Shule nyingi kongwe na taasisi mbalimbali za huduma zilianzishwa na taasisi za dini kabla hata ya Serikali kuendelea kuzijenga na kuzisimamia,” amesema Dkt. Mwigulu.

Aidha, Waziri Mkuu amesema kuanzia mwaka 2028 Serikali itaanza rasmi utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka 10 kwa watoto wote wa Kitanzania kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne kwa lengo la kuongeza ujuzi na kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea.

“Hatusemi shule ya msingi iwe miaka 10, tunasema elimu ya lazima kwa mtoto wa Kitanzania iwe miaka 10 ili watoto wetu wapate maarifa na ujuzi wa kutosha kwa maisha yao ya baadaye,” amesema.

Dkt. Mwigulu amesema hatua hiyo pia inalenga kupunguza changamoto za watoto kuacha shule katika umri mdogo pamoja na kukabiliana na changamoto za ndoa za utotoni kwa kuhakikisha watoto wanabaki shuleni kwa muda mrefu zaidi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amepongeza KKKT Dayosisi ya Iringa kwa kuendelea kuwahudumia watoto yatima na watu wenye mahitaji maalum huku akieleza kuwa Serikali inaendelea kufanya maboresho ya sera na mifumo ya utoaji wa huduma kwa makundi hayo.

Amesema Serikali imeanza kufanya marekebisho ya mfumo wa utoaji wa mikopo kwa watu wenye ulemavu ili hata mtu mmoja mmoja aweze kunufaika badala ya kulazimika kuunda vikundi.

“Tunataka kujenga mfumo unaowatambua watu wenye mahitaji maalum kwa utu wao na kuhakikisha wanapata huduma na msaada stahiki bila usumbufu,” amesema.

Kwa upande wake, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Iringa, Dkt. Blaston Gavile amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Waziri Mkuu katika kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi pamoja na kuendelea kusimamia maendeleo ya Taifa kwa karibu.

“Hakika kwa kipindi hiki kifupi tangu kuteuliwa kwako tumeona moyo wako wa kuwatumikia Watanzania. Umetenga muda wako kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua kwa busara, uelewa na hekima kubwa,” amesema Dkt. Gavile.

Aidha, amesema KKKT inaunga mkono maono ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi imara, huduma bora za jamii na maendeleo endelevu kwa Watanzania wote.

No comments:

Post a Comment