
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Raphael Chibunda, amesema panya Magawa, aliyefunzwa na SUA kwa kushirikiana na shirika la APOPO, ameacha historia kubwa nchini Cambodia baada ya kusaidia kugundua mabomu ya ardhini na hatimaye kujengewa mnara wa kumuenzi katika mji wa Siem Reap.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Agosti 31,2026, Profesa Chibunda amesema panya wanaotumika katika mradi huo ni panya wa asili wa Tanzania, ambao awali walikamatwa katika milima ya Uluguru mkoani Morogoro na sasa wanaendelea kuzalishwa na kufundishwa katika kituo hicho.
Amesema SUA imeweka mfumo maalumu wa kuwahudumia panya hao katika hatua mbalimbali za maisha yao, kuanzia kuzaliwa, mafunzo hadi kustaafu.
“Ukija pale kwetu utakuta tuna wodi ya wazazi, tuna wale ambao wanaanza mafunzo, kuna waliohitimu mafunzo, lakini vilevile tuna banda ambalo ni la panya wastaafu. Wako pale wanapata pensheni,” amesema Profesa Chibunda.
Amesema Magawa alikuwa miongoni mwa panya waliopelekwa nchini Cambodia, moja ya mataifa yenye changamoto ya mabomu ya ardhini kutokana na historia ya migogoro iliyowahi kutokea nchini humo.
Profesa Chibunda amesema Tanzania haina tatizo kubwa la mabomu ya ardhini, hivyo panya wanaofundishwa nchini hutumika zaidi kwa kushirikiana na mataifa yenye changamoto hiyo.
“Kwa sababu sisi tuna bahati na inabidi tuendelee kumshukuru Mungu kwamba nchi yetu haina tatizo la mabomu ya kutegwa ardhini. Kwa hiyo wenzetu nchi ambazo zinazo matatizo ndio mradi tunakwenda, ndio partner wetu, ndio washiriki wetu. Kwa hiyo Cambodia ni kati ya hizo nchi,” amesema.
Kwa mujibu wa Profesa Chibunda, Magawa alifanya kazi kubwa nchini Cambodia na kuvunja rekodi baada ya kufanikiwa kugundua mabomu mengi ya ardhini kuliko panya wengine waliowahi kufanya kazi hiyo.
Magawa alifanya kazi nchini Cambodia kuanzia mwaka 2016 hadi alipostaafu mwaka 2021, ambapo alifanikiwa kugundua zaidi ya mabomu 100 ya ardhini na mabaki ya vilipuzi, huku akisaidia kusafisha zaidi ya mita za mraba 141,000 za ardhi, sawa na takribani viwanja 20 vya mpira wa miguu.
Kutokana na mafanikio hayo, Magawa alitambuliwa kimataifa na kutunukiwa Medali ya Dhahabu ya PDSA kwa ushujaa, ikiwa ni heshima kwa wanyama walioonyesha ujasiri na mchango mkubwa katika huduma kwa binadamu.
Profesa Chibunda amesema panya hao wana muda mfupi wa kuishi, ambapo wanapofikia takribani miaka minane huanza kuingia katika hatua ya uzee.
Amesema Magawa alifikia umri huo na baadaye alifariki, licha ya kuwa alikuwa ameshaacha historia kubwa kutokana na kazi yake ya kugundua mabomu.
“Panya wale umri wao ni miaka minane. Akifika tisa ni mzee kweli hata hana meno. Kwa hiyo Magawa umri wake ukafika na bahati mbaya akafariki,” amesema.
Profesa Chibunda amesema baada ya kifo cha Magawa, kulikuwa na wazo la kumrudisha Tanzania ili azikwe nchini, lakini mpango huo haukuweza kutekelezwa kutokana na changamoto za vibali na taratibu za usafirishaji.
Amesema pamoja na kushindikana kwa mpango huo, upande wa Cambodia uliamua kumuenzi kwa kumjengea mnara mkubwa katika mji wa Siem Reap.
“Sasa je, tungemleta akazikwa huku? Sisi tunasema ingeweza kuanza, lakini kwa wakati ule logistics kama iligoma hivi kwa sababu vibali vilivyokuwa vinahitajika, na wenzetu kule wakakosa uvumilivu wa kuendelea kumtunza,” amesema.
Mnara wa Magawa wenye urefu wa takribani mita 2.2 ulizinduliwa Aprili 3, 2026, katika mji wa Siem Reap nchini Cambodia, ukiwa kumbukumbu ya mchango wake katika shughuli za kugundua mabomu ya ardhini.
Mnara huo unaonyesha Magawa akiwa amevaa medali yake, huku sehemu ya chini ikiwa na mfano wa bomu la ardhini na vipande vya vilipuzi vilivyoondolewa na kuzimwa.
Hatua hiyo imeufanya mchango wa Magawa kuendelea kukumbukwa na wananchi pamoja na wageni wanaotembelea eneo hilo.
Profesa Chibunda amesema pamoja na mnara uliojengwa Cambodia, SUA pia inaendelea kumuenzi Magawa ndani ya chuo hicho mkoani Morogoro kwa kutaja barabara maalumu kwa jina lake.
“Lakini wamemjengea mnara mkubwa kule, na sisi ukija chuoni kwetu hata tuna barabara mahsusi linaitwa Barabara la Magawa,” amesema.
Amesema jamii ya watafiti wanaohusika na eneo hilo pia huadhimisha siku ya kifo cha Magawa kama sehemu ya kumkumbuka na kutambua mchango wake.
Profesa Chibunda amesema matumizi ya panya hao hayaishii katika kugundua mabomu ya ardhini, bali pia wanatumika katika shughuli za afya, hususan kusaidia kugundua vimelea vya kifua kikuu (TB).
Amesema panya hao husaidia kutambua baadhi ya sampuli za makohozi ambazo hazikubainika kuwa na maambukizi kupitia vipimo vya kawaida vya darubini.
Sampuli zinazotambuliwa na panya hao huweza kurejeshwa hospitalini kwa ajili ya vipimo vya kina zaidi, hatua inayosaidia kuongeza uwezekano wa kuwabaini wagonjwa ambao hawakugunduliwa katika uchunguzi wa awali.
Katika hatua nyingine, Profesa Chibunda amesema SUA inaendelea kutumia teknolojia za kisasa katika kuimarisha kilimo na ufugaji.
Amesema chuo hicho kinatumia ndege zisizo na rubani (droni) katika mafunzo na shughuli mbalimbali za kilimo, ikiwemo unyunyiziaji wa dawa na uwekaji wa mbolea mashambani.
Aidha, SUA imebuni programu mbalimbali za simu zinazolenga kuwasaidia wakulima na wafugaji katika shughuli zao.
Miongoni mwa ubunifu huo ni programu inayomsaidia mfugaji wa samaki kuhesabu idadi ya vifaranga kwa kutumia picha, ambapo mfumo hutoa makadirio ya idadi yao na hivyo kupunguza usumbufu unaoweza kujitokeza wakati wa kuhesabu kwa njia za kawaida.
Profesa Chibunda amesema SUA pia imefanya mabadiliko katika mitaala yake ili kuwaandaa wahitimu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.
Amesema wanafunzi sasa watafanya mafunzo ya vitendo kwa kipindi cha miezi sita mfululizo, badala ya mafunzo ya muda mfupi, ili kuwawezesha kupata uzoefu wa kutosha katika mazingira halisi ya kazi.
Amesema mafunzo hayo yatahusisha kufanya kazi na wakulima pamoja na viwanda vinavyohusiana na taaluma zao.
Aidha, amesema asilimia 20 ya ufundishaji inatarajiwa kufanywa na wataalamu kutoka sekta binafsi na viwandani, kwa lengo la kuwapa wanafunzi ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.
SUA pia imeunda kamati maalumu ya kuimarisha ushirikiano kati ya chuo na sekta binafsi ili kuhakikisha elimu inayotolewa inaendana na mahitaji ya soko na jamii.
Amesema simulizi ya Magawa ni sehemu ya mafanikio yanayoonyesha uwezo wa Tanzania katika utafiti na matumizi ya wanyama wa asili kutatua changamoto za kibinadamu.
“Kwa hiyo mimi nipende labda tungepata sasa hata ninyi waandishi wa habari wa kuandika habari njema ya hawa panya lakini tukampa kipaimbele Magawa, ili habari hii sije kesho na keshokutwa ikasahaulika,” amesema.
Kutoka milima ya Uluguru mkoani Morogoro hadi Cambodia, Magawa ameacha urithi unaoendelea kuenziwa kupitia mnara nchini Cambodia na Barabara ya Magawa ndani ya SUA, huku panya wengine wakiendelea kufundishwa kwa ajili ya kazi za kibinadamu.

No comments:
Post a Comment