TALGWU YAWASILISHA CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI WAFANYAKAZI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, September 17, 2026

TALGWU YAWASILISHA CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI WAFANYAKAZI



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) kimewasilisha changamoto saba zinazowakabili watumishi wa umma, kikiiomba Serikali kuzitafutia ufumbuzi ili kuboresha mazingira ya kazi, maslahi ya watumishi na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Ombi hilo limetolewa leo Septemba 17,2026 jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu wa TALGWU, Wandiba Ngocho, wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho uliohudhuriwa na viongozi wa Serikali pamoja na wajumbe wa vyama vya wafanyakazi kutoka ndani na nje ya nchi.

Ngocho amesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili watumishi ni ucheleweshaji wa fedha za likizo, ambapo baadhi ya watumishi hupokea stahiki hizo kwa awamu au baada ya muda uliopangwa.

Ameitaja pia changamoto ya ucheleweshaji wa malipo ya posho na leseni za huduma kwa watumishi wa kada za afya, hali ambayo amesema inahitaji kushughulikiwa ili kuhakikisha watumishi wanapata stahiki zao kwa wakati.

Katika changamoto nyingine, TALGWU imeeleza kuwa baadhi ya watumishi hukumbana na ucheleweshaji wa malipo ya stahiki za uhamisho wanapohamishwa kutoka kituo kimoja cha kazi kwenda kingine.

Aidha, chama hicho kimeeleza kuwepo kwa changamoto katika utekelezaji na matumizi ya mfumo wa Upimaji Utendaji Kazi (PEPMIS), huku kikihitaji maboresho yatakayorahisisha utekelezaji wa mfumo huo kwa watumishi.

Changamoto nyingine ni pamoja na miundo ya utumishi na mchakato wa kubadilishiwa kada (re-categorization), ambapo baadhi ya watumishi hukumbana na vikwazo katika kubadilishiwa kada kulingana na elimu na ujuzi walioupata.

TALGWU pia imewasilisha changamoto ya kutofanya kazi kwa ufanisi kwa baadhi ya Mabaraza ya Wafanyakazi katika halmashauri na taasisi, jambo ambalo chama hicho kinaona linapaswa kushughulikiwa ili kuongeza ushirikishwaji wa wafanyakazi katika masuala yanayohusu ajira zao.

Pamoja na hayo, chama hicho kimeomba kuendelea kuboreshwa kwa mazingira ya kazi na maslahi ya watumishi, hususan wale wanaotekeleza majukumu katika maeneo ya pembezoni.

Kwa mujibu wa Ngocho, utatuzi wa changamoto hizo utasaidia kuongeza morali na ari ya watumishi, jambo litakaloleta ufanisi zaidi katika utekelezaji wa majukumu na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.


Aidha, amezipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kusikiliza na kushughulikia changamoto za wafanyakazi, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha zaidi mfumo wa majadiliano endelevu kati ya Serikali na wafanyakazi.






No comments:

Post a Comment