BoT YAWAJENGEA UWEZO WAANDISHI WA HABARI KUHUSU UCHUMI NA FEDHA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, November 4, 2026

BoT YAWAJENGEA UWEZO WAANDISHI WA HABARI KUHUSU UCHUMI NA FEDHA



Na OKULY BLOG, DAR ES SALAAM



Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Rahma Salim Mahfoudh, amesema ni muhimu kwa waandishi wa habari kuwa na uelewa mpana wa masuala ya uchumi na fedha ili waweze kuripoti kwa usahihi na kuelimisha wananchi kuhusu mwenendo wa uchumi nchini.

Dkt. Mahfoudh ameyasema hayo leo Novemba 4,2026 jijini Dar es Salaam wakati akifungua semina ya siku tatu kwa waandishi wa habari kutoka mikoa mbalimbali nchini, inayolenga kuwajengea uwezo kuhusu sera ya fedha, majukumu ya Benki Kuu na masuala mbalimbali ya sekta ya fedha.

Amesema mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa wa waandishi wa habari kuhusu majukumu na shughuli za Benki Kuu ya Tanzania ili kuwawezesha kuandika na kuripoti habari zinazohusu uchumi na fedha kwa usahihi na weledi.

Aidha, amesema semina hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano kati ya BoT na vyombo vya habari katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na elimu kuhusu masuala ya uchumi na fedha.

Ameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo, waandishi wa habari wanatarajiwa kuongeza uwezo wa kuchambua masuala ya kiuchumi na kuandaa habari pamoja na makala zenye ubora zinazohusu sekta ya fedha.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi katika semina hiyo Meneja mkuu wa mawasiliano wa BOT Victoria Msina amesema kupitia mafunzo hayo, waandishi wa habari wanatarajiwa kuongeza uwezo wa kuchambua masuala ya kiuchumi na kuandaa habari pamoja na makala zenye ubora zinazohusu sekta ya fedha.

Semina hiyo imewakutanisha wahariri na waandishi wa habari kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Zanzibar, Dodoma, Pwani na Morogoro, ambapo wataalamu kutoka Benki Kuu wanatoa mada mbalimbali zinazohusu shughuli na mifumo ya sekta ya fedha nchini.

Miongoni mwa mada zinazofundishwa ni utekelezaji wa sera ya fedha, matumizi ya viwango vya riba, dhamana za Serikali na mchango wake katika kuimarisha masoko ya fedha.

Mada nyingine zinahusu mifumo ya malipo salama inayotumiwa na Benki Kuu, mifumo ya kitaifa ya malipo pamoja na masuala ya kisheria na kiutendaji yanayohusiana na mifumo hiyo.


Benki Kuu ya Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari katika mikoa mbalimbali nchini ili kuongeza uelewa wao kuhusu masuala ya uchumi na fedha na kuwawezesha kutekeleza jukumu lao la kuhabarisha na kuelimisha umma kwa ufanisi.





No comments:

Post a Comment