
Na Okuly Julius, OKULY BLOG – DAR ES SALAAM
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa dhamana za mikopo zenye thamani ya Shilingi trilioni 1.6 zilizowezesha wafanyabiashara na wajasiriamali kupata mikopo yenye thamani ya Shilingi trilioni 2.1 kupitia taasisi mbalimbali za fedha nchini.
Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Fedha wa BoT, Bi. Gloria Chellunga, amesema hayo leo, Novemba 5, 2026, wakati akiwasilisha mada kuhusu utendaji wa Mfuko wa Dhamana ya Mikopo na wigo wake wa kisheria katika semina ya siku tatu kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Amesema mfumo huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuwawezesha wafanyabiashara na wajasiriamali wenye miradi yenye tija kupata mikopo kutoka katika taasisi za fedha, licha ya kukabiliwa na changamoto ya kutokuwa na dhamana ya kutosha inayotakiwa na wakopeshaji.
Ameeleza kuwa Serikali imeanzisha mifuko miwili ya dhamana ya mikopo inayosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania, ambayo inalenga kuziba pengo la upatikanaji wa mikopo kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wanaokidhi vigezo vya kukopeshwa lakini wanakosa dhamana ya kutosha.
Mifuko hiyo ni Mfuko wa Dhamana ya Mikopo kwa Mauzo ya Nje (Export Credit Guarantee Scheme – ECGS), ulioanzishwa Julai 2002, na Mfuko wa Dhamana ya Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (Small and Medium Enterprises Credit Guarantee Scheme – SMECGS), ulioanzishwa Septemba 2005.
Akifafanua utaratibu wa kupata dhamana hizo, Chellunga amesema maombi huwasilishwa na benki au taasisi ya fedha inayokusudia kumkopesha mteja baada ya kufanya tathmini na kubaini kuwa ana uwezo wa kukidhi masharti mengine ya mkopo, lakini ana upungufu wa dhamana.
Amesema katika utaratibu huo, taasisi ya fedha huwasilisha barua rasmi Benki Kuu ikieleza taarifa za mwombaji, kiasi cha mkopo anaohitaji pamoja na kiwango cha upungufu wa dhamana, huku ikiomba BoT idhamini sehemu ya mkopo huo.
Amefafanua kuwa baada ya kupokea maombi hayo, Benki Kuu hufanya tathmini ya kina ili kujiridhisha kuhusu uwezo wa mradi husika kuzalisha mapato na kurejesha mkopo unaoombwa.
Amesisitiza kuwa dhamana hizo hazimaanishi kuwa mikopo inatolewa bila tathmini, bali ni utaratibu unaosaidia kupunguza hatari kwa taasisi za fedha na kuongeza fursa za mikopo kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wenye miradi inayotekelezeka.
Kupitia mifuko hiyo, Serikali inalenga kuimarisha shughuli za biashara, uzalishaji na uwekezaji, kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za kifedha nchini.


No comments:
Post a Comment