JAJI MSTAAFU HAMISA KALOMBOLA : WATUMISHI WAHIMIZWA KUSIMAMIA RASILIMALI ZA UMMA KWA UWAZI NA UWAKIBIKAJI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, November 5, 2026

JAJI MSTAAFU HAMISA KALOMBOLA : WATUMISHI WAHIMIZWA KUSIMAMIA RASILIMALI ZA UMMA KWA UWAZI NA UWAKIBIKAJI


Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu Hamisa Kalombola, amewataka watumishi wa taasisi hiyo kusimamia kwa uangalifu rasilimali za umma, kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, ili kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji.

Akizungumza leo Novemba 05,2026 jijini Dodoma wakati wa kufungua Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Umma, Kalombola amesema usimamizi wa pamoja wa masuala ya fedha ni muhimu katika kupunguza malalamiko, migogoro na mianya ya upotevu wa rasilimali.

Amesema baraza hilo ni jukwaa muhimu linalounganisha uongozi na wafanyakazi, hivyo linapaswa kutumika kujadili masuala mbalimbali ya taasisi, ikiwemo utekelezaji wa bajeti na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho.

Pia Kalombola amewahimiza wajumbe wa baraza hilo kushiriki kikamilifu katika majadiliano kwa kutoa hoja, maoni na mapendekezo yenye tija, akisisitiza kuwa kila mchango una nafasi katika kuboresha utendaji wa taasisi.

Aidha, amesema uongozi wa tume uko tayari kusikiliza na kufanyia kazi mapendekezo ya wafanyakazi, huku akiahidi ushirikiano katika kutatua changamoto zinazohitaji msaada kutoka mamlaka nyingine za utumishi wa umma.

Katika mkutano huo, wajumbe wanatarajiwa kupitia taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Tume kwa mwaka wa fedha 2025/2026, pamoja na kujadili masuala ya uwakilishi wa wafanyakazi na maazimio ya kuboresha utendaji.


No comments:

Post a Comment