
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Mei 06, 2025 limepitisha kwa kishindo Bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ya Shilingi trilioni 2.28 baada ya mjadala wa kina uliohitimishwa na Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha mjadala huo, Waziri Ulega amesema bajeti ya Wizara hiyo imeongezeka kutoka trilioni 1.6 hadi trilioni 2.28, sawa na ongezeko la asilimia 28, hatua ambayo inalenga kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maendeleo katika Sekta ya Ujenzi.
“Kazi kubwa ya ujenzi katika nchi yetu imefanyika na tunaahidi kuendelea kujenga barabara bila kuchoka, bila kusimama,” alisema Waziri Ulega huku akieleza kuwa wizara hiyo itaendelea kufanya kazi usiku na mchana kutatua changamoto za miundombinu nchini.
Katika maelezo yake, Waziri Ulega ameeleza kuwa kuanzia mwaka 2021 hadi sasa, jumla ya Shilingi trilioni 2.5 zimeshalipwa kwa wakandarasi mbalimbali.
Pia amebainisha kuwa kila mwezi, Wizara ya Fedha imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kuwalipa wakandarasi wa ndani na nje wanaotekeleza miradi ya barabara.
Aidha, ameeleza kuwa miradi 81 ya dharura yenye thamani ya Shilingi bilioni 559.6 inatekelezwa, ambapo miradi 70 yenye thamani ya bilioni 414 imetekelezwa na wakandarasi wazawa.
Pia amegusia barabara ya Mtwara – Mingoyo – Masasi ambapo kipande cha kutoka Mtwara hadi Mnazi Mmoja kimeshasainiwa mkataba na mkandarasi, na fedha za awali zimeshatolewa. Aidha, malipo ya mkandarasi wa kipande cha Mingoyo hadi Masasi yanatarajiwa kufanyika ndani ya wiki mbili zijazo.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya. Hakika hakuna tunachomdai, ameonyesha uongozi wa mfano katika kuimarisha miundombinu ya nchi yetu,” alisema Waziri Ulega.
Katika bajeti hiyo, jumla ya Shilingi 2,280,195,828,000 zimetengwa ambapo Shilingi 90,468,270,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya wizara na taasisi zake, na Shilingi 2,189,727,558,000 zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Bunge limepitisha bajeti hiyo kwa sauti ya pamoja, ikiwa ni ishara ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya usafiri na kuimarisha uchumi wa taifa.









No comments:
Post a Comment