“Nilipoambiwa na viongozi wangu wa kazi kuwa natakiwa kwenda mkoani Singida kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi mwaka huu ambapo nitakabidhiwa cheti na zawadi ya kuwa mfanyakazi bora wa Barrick Bulyanhulu wa mwaka huu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Samia Suluhu Hassan,nilibaki na mshangao bila kuamini nilichoambiwa”.
Siku ya tukio hilo nilivyopangwa kwenye orodha ya wafanyakazi bora kutoka taasisi mbalimbali tuliokabidhiwa vyeti na Rais mpaka nilipomsogelea na kukabidhiwa zawadi na cheti nilikuwa kama vile niko ndotoni, baada ya kupokea zawadi wafanyakazi wenzangu walinipokea kwa furaha ndipo niliamini kilichotokea mpaka nikawa najiuliza nitamlipa nini mwajiri wangu Barrick aliyenifanyia mambo haya makubwa”, anasema Michael Weruma.
Michael Werema ni mwendeshaji wa moja ya mitambo ya kisasa katika mgodi wa Barrick ambaye amekuwa na nia ya kujifunza kwa bidii kazi za migodini tangia alipoajiriwa,kufanya kazi kwa bidii,ushirikiano mzuri na wenzake pia amekuwa na rekodi nzuri ya kuzingatia kanuni za usalama katika utendaji wake wa kazi wa kila siku.
Katika mahojiano yaliyofanyika mapema wiki iliyopita,Weruma mwenye umri wa miaka 42 alisema japo amesomea taaluma ya biashara na masoko alijikuta tangu akiwa na umri mdogo akiwa na ndoto ya kufanya kazi kwenye migodi kutokana na kuvutiwa na ndugu yake aliyekuwa anafanya kazi katika moja ya mgodi hapa nchini.
Alisema alijiunga na Kampuni ya Barrick, katika Mgodi wa Bunyanhulu, mnamo mwaka 2021 kama msaidizi mtoa huduma (service Man) Alikuwa akijifunza kila siku chini wa usimamizi wa viongozi wake na kuendelea kupanda siku hadi siku mpaka kufikia mahali ambapo anaweza kufanya kazi bila msimamizi ambapo kwa sasa anamudu kuendesha mtambo wa kuweka vizuri mazingira ya uchimbaji ujulikanao kama Boom Truck ambao pia unachoronga miamba.
“Kwenye maeneo ya Migodi nimeweza kukutana na watu wengi kutoka Mataifa mbalimbali ambapo nimejifunza mambo mengi kuhusiana na fani yangu kwendana na viwango vya juu vya utendaji kazi vya kampuni ya Barrick. Namudu vizuri kazi yangu na kufuata taratibu sambamba na kuhakikisha malengo na matarajio yaliyowekwa na mwajiri wangu yanafikiwa,” alisema Weruma.
Anasema amefurahi mchango wake wa kazi unathaminiwa na kampuni ambapo ametangazwa kuwa Mfanyakazi Bora wa Mwaka wa Mgodi wa Bulyangulu kwa 2025, hatua ambayo alidai imezidi kumpa moyo wa kufanya kazi yake kwa bidii zaidi.
Alipoulizwa siri kubwa ya mafanikio hayo, alisema yanatokana na kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wafanyakazi wenzake ambao wakati wote wamekuwa wakimpatia ushirikiano mkubwa pia kampuni imekuwa ikiandaa mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo anadai yamemsaidia katika safari yake ya mafanikio.
Vilevile aliongeza kuwa uwekezaji mkubwa wa Barrick, kwenye matumizi ya teknolojia za kisasa za kimataifa na mifumo ya kidigitali kwenye migodi yake, kumemwezesha kujua mambo mengi ya matumizi ya vifaa vya kisasa na kujenga mazingira bora ya kufanyia kazi yenye viwango vya juu vya kimataifa na vyenye usalama zaidi.
“Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru viongozi wangu na menejimenti nzima hususani msimamizi wangu wa kitengo cha ujenzi (construction) kwa kunipa nafasi kunijenga mpaka napata nafasi ya kuwa mfanyakazi bora wa mwaka 2025 nawashukuru sana,” alisema Weruma.
Kuhusu changamoto anazokumbana nazo katika kazi yake,alisema ni za kawaida kwa kuwa hakuna kazi yoyote isiyokuwa na changamoto.”Changamoto kwangu huwa nazichukulia kama ni sehemu ya kujifunza mambo mapya” alisema.
Weruma ambaye kabla hajajiunga na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu alifanya kazi kwenye kampuni ya simu za mikononi ya Tigo mkoani Dodoma ana stashahada ya Masoko kutoka Shirika la Elimu Tanzania.
Weruma, alitoa wito kwa Wafanyakazi wenzake na wote wanaotaka kuingia fani hiyo kuhakikisha wanakuwa na weledi katika fani pia wafanye kazi kwa umakini na ufanisi wakati wote.
Kuhusiana na malengo yake ya baadaye alisema anataka kujiendeleza zaidi kitaaluma ili aweze kuwa na uwezo wa kwendana na mabadiliko ya teknolojia katika tasnia ya uchimbaji wa madini na kufikia viwango vya kufanya kazi kwenye migodi yenye viwango vya kimataifa nje ya Tanzania kama ilivyo migodi ya kampuni ya Barrick.
No comments:
Post a Comment