MIRADI YA MAJI INAENDELEA KUJENGWA NCHINI KOTE-MAJALIWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, May 18, 2025

MIRADI YA MAJI INAENDELEA KUJENGWA NCHINI KOTE-MAJALIWA


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea na ujenzi wa miradi ya maji katika maeneo yote nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo karibu na makazi yao.

Ameyasema hayo leo (Jumapili, Mei 18, 2025) wakati akizungumza na wananchi katika Eneo la Hungumalwa wilayani Kwimba, Mwanza baada ya kuzindua mradi wa maji Hungumalwa akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mwanza. Mradi huo wa maji wa Hungumalwa ulianza kutekelezwa tarehe Machi 08, 2022 na ulikamilika Agosti 15, 2024.

Mheshimiwa Majaliwa amewasisitiza wananchi kuendelea kuiamini na kushirikiana na Serikali ambayo imedhamiria kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao. Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na ya elimu, maji, afya na ujenzi wa barabara.

”Tutaendelea kusimamia maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na tutaendelea kutekeleza ilani kwa vitendo. Kwenye elimu tunaendelea kukarabati na kuimarisha shule zote za msingi na sekondari. Tutawahudumia wananchi wala msiwe na mashaka. Suala la maji tunaendelea kuhakikisha yanapatikana maeneo yote.”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi ambao bado hawajaunganisha umeme katika majumba yao wafanye hivyo ili waweze kunufaika na huduma hiyo.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Mwanza, Mhandisi Godfrey Sanga amesema mradi huo umetekelezwa na mkandarasi Emirate Builders Company Limited na kusimamiwa na wataalam wa RUWASA.

Amesema gharama ya mkataba ni shilingi bilioni 11, ambapo mpaka sasa kazi zote zimekamilika kwa thamani ya shilingi bilioni 10 na kufanya salio katika mkataba wa ujenzi wa mradi huo kuwa ni shilingi milioni 201.

Meneja huyo ametaja kazi zilizopangwa kufanyika katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa tangi moja lenye ujazo wa lita milioni moja, ununuzi wa mabomba na viungio vyake km 54.817, uchimbaji na ufukiaji mitaro yenye urefu wa km 54.817, kuunganisha maji kwa wateja wa majumbani 500, ujenzi wa ofisi ya chombo cha watumia maji ngazi ya jamii na ujenzi wa nyumba ya mlinzi, ambapo kazi zote zimekamilika.

Mradi wa maji kijiji cha Hungumalwa ni moja kati ya miradi iliyotekelezwa kupitia fedha za ndani za Serikali (GoT). Katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita, Wilaya ya Kwimba inatekeleza jumla ya miradi 20 yenye thamani ya Sh. 32,388,599,515.96 ambapo jumla ya fedha Sh. 20,961,344,300.48 zimeshatumika. Mradi huu wa Hungumalwa unahudumia jumla ya wakazi 24,349 (sensa 2022) wa vijiji vya Hungumalwa, Buyogo, Ilula na Kibitilwa. Chanzo cha maji cha mradi huu ni ziwa Victoria.

No comments:

Post a Comment