Na Okuly Julius _ DODOMA
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Ashatu Kijaji amesema
wanatarajia kuzindua Kampeni ya Chanjo ya Mifugo Kitaifa kati ya mwezi Mei hadi Juni, 2025 ambapo tayari imenunua zaidi ya dozi milioni 19 za chanjo ya Homa ya Mapafu ya Ng’ombe (CBPP), dozi zaidi ya milioni 17 za chanjo ya Sotoka kwa Mbuzi na Kondoo, na dozi milioni 40 za chanjo dhidi ya Kideri/Mdondo (ND), Ndui, na Mafua ya Kuku kwa ajili ya kuchanja kuku wa asili.
Dkt. Kijaji ametoa kauli hiyo leo Mei 6,2025 jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Kijaji amesema kuwa zoezi hilo la chanjo litaiwezesha Tanzania kukidhi masharti ya kimataifa ya biashara ya mifugo na mazao yake, kwa mujibu wa Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH), Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), na Shirika la Biashara Duniani (WTO).
“Katika kuimarisha afya ya mifugo nchini, Serikali imenunua jumla ya dozi 19,099,100 za chanjo ya CBPP kwa ajili ya kuchanja ng’ombe 19,099,100; dozi 17,224,200 za chanjo ya Sotoka kwa ajili ya mbuzi na kondoo; na dozi 40,000,000 za chanjo kwa kuku wa asili dhidi ya Kideri, Ndui na Mafua,” amesema Dkt. Kijaji.
Ameongeza kuwa Serikali imenunua zaidi ya hereni za kidijitali milioni 36 kwa ajili ya utambuzi wa ng’ombe, mbuzi na kondoo watakaopatiwa chanjo hizo. Lengo ni kuhakikisha kila mnyama anatambulika, hatua itakayowezesha kukidhi matakwa ya soko la kikanda na kimataifa, pamoja na kusaidia udhibiti wa magonjwa, ufuatiliaji wa mifugo, kudhibiti wizi, na kuwezesha wafugaji kupata mikopo na bima.
Kuhusu biashara ya nyama, Dkt. Kijaji amesema kuwa mauzo ya nyama nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 1,774 zenye thamani ya shilingi bilioni 9.86 mwaka 2020/2021 hadi tani 13,745.38 zenye thamani ya shilingi bilioni 147.13 mwaka 2024/2025. Kwa kipindi cha miaka minne, jumla ya tani 40,635 za nyama zenye thamani ya shilingi bilioni 414.37 zimeuzwa nje ya nchi.
Amezitaja nchi zinazonunua nyama kutoka Tanzania kuwa ni Bahrain, Comoro, Hong Kong, Jordan, Kenya, Kuwait, Oman, Qatar, Rwanda, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Vietnam.
Akizungumzia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Kijaji amesema sekta hiyo imezalisha ajira za moja kwa moja kwa wavuvi 201,661 na wakuzaji viumbe maji 49,084, huku takriban Watanzania milioni sita wakijihusisha na shughuli mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa uvuvi.
No comments:
Post a Comment