WAELIMISHA RIKA WATAKIWA KUTUMIA MBINU ZA KISASA KATIKA KUELIMISHA MASUALA YA AFYA KAZINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 15, 2025

WAELIMISHA RIKA WATAKIWA KUTUMIA MBINU ZA KISASA KATIKA KUELIMISHA MASUALA YA AFYA KAZINI



NA. MWANDISHI WETU - MOROGORO


Waelimisha rika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) watakiwa kutumia mbinu mbadala na zinazokwenda na mazingira ya sasa katika kufikisha elimu ya afya kwa watumishi wenzao kazini huku wakijitolea kwa uzalendo na weledi ili kuendelea kuwa na mazingira mazuri ya utendaji wa kazi kwa kuzingatia afya zao.

Hayo yamebainishwa Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Bw. Eleuter Kihwele kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim James Yonazi hii leo Mei 15, 2025, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kwa waelimisha rika mahala pa kazi, yanayofanyika mjini Morogoro.

Kihwele amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo waelimisha rika katika utoaji wa elimu, hasa katika kipindi hiki ambapo jamii inakumbwa na ongezeko la magonjwa yasiyoambukizwa pamoja na changamoto nyingine za kiafya.

“Mafunzo haya yatakuwa na mada muhimu. Zingatieni ili kuwawezesha watumishi wenzenu kupata uelewa wa kina kuhusu masuala ya VVU na UKIMWI pamoja na magonjwa yasiyoambukizwa,” alisema Bw. Kihwele.

Aidha, amepongeza maandalizi ya mafunzo hayo, akisisitiza kuwa yatatoa mwanga na mwelekeo mpya wa kuhakikisha Ofisi ya Waziri Mkuu inakuwa mfano wa kuigwa katika kueneza elimu ya afya kwa watumishi wake.

Kwa mujibu wa Kihwele, mafunzo kwa waelimisha rika hufanyika kila mwaka ili kutathmini utekelezaji wa mwongozo uliopo, kubaini changamoto na kuja na mikakati bora ya kudhibiti magonjwa katika Idara na Vitengo husika.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Menejimenti ya Anuai za Jamii, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora;Bi. Mwanaamani Mtoo, ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendeleza utekelezaji wa mwongozo wa waelimisha rika kwa mafanikio makubwa.

“Sisi kama wasimamizi wa rasilimali watu, tunawapongeza kwa hatua mliyoifikia. Kuendeleza juhudi hizi ni hatua muhimu ya kudhibiti maambukizi ya VVU na UKIMWI pamoja na magonjwa yasiyoambukizwa kazini,” alisema Bi. Mtoo.

Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu imeendelea kuweka kipaumbele katika afya na ustawi wa watumishi wake, ikiwemo kutoa mafunzo ya stadi za afya kwa waelimisha rika na kuwawezesha kuwa mabalozi wa mabadiliko ya kiafya katika maeneo yao ya kazi.







No comments:

Post a Comment