WAZIRI DKT. GWAJIMA AISHUKURU SERIKALI YA FINLAND KWA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KATIKA UWEZESHAJI WANAWAKE KIUCHUMI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 16, 2025

WAZIRI DKT. GWAJIMA AISHUKURU SERIKALI YA FINLAND KWA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KATIKA UWEZESHAJI WANAWAKE KIUCHUMI


Na WMJJWM – Dar es Salaam


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (Mb), ametoa salamu za shukrani kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia ziara rasmi ya Mhe. Rais Alexander Stubb wa Jamhuri ya Finland katika Soko la Machinga Complex jijini Dar Es Salaam.

Ziara hiyo ya kihistoria imetajwa kuwa ishara ya urafiki wa kudumu kati ya Tanzania na Finland, ambao mwaka huu unatimiza miaka 60 ya mahusiano ya kidiplomasia. Akitoa Salamu hizo Dkt. Gwajima amesisitiza kuwa hatua hiyo inaakisi dhamira ya dhati ya mataifa haya mawili katika kuendeleza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake, hasa walioko katika sekta isiyo rasmi.

"Kwa niaba ya Serikali, tunawashukuru sana kwa kuonesha mshikamano wenu na kuunga mkono juhudi zetu katika kuwawezesha wanawake. Hii ni hatua kubwa kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi," amesema Dkt. Gwajima

Dkt. Gwajima ameleza kuwa Tanzania inatambua umuhimu wa kushughulikia changamoto za kijinsia kama njia ya kufanikisha maendeleo endelevu. Amesisitiza kuwa wanawake walioko kwenye sekta isiyo rasmi, hususan wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga, ni nguzo muhimu ya uchumi wa taifa.

"Ziara hiu ni uthibitisho wa urafiki wa dhati kati ya mataifa yetu na dhamira ya pamoja ya kuendeleza haki za wanawake. Tunashukuru kwa kuendelea kutuunga mkono katika kusukuma mbele ajenda ya usawa wa kijinsia," amesema Dkt. Gwajima.

Naye Rais wa Finland Mhe. Alexander Stubb ameleza kuvutiwa na uthubutu pamoja na juhudi za wanawake wanaojishughulisha na biashara ndogondogo na kupongeza hatua zinazochukuliwa na Tanzania katika kuimarisha haki za wanawake. Pia ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika masuala ya kijinsia, maendeleo ya jamii na ustawi wa wanawake, hasa wale waliopo katika ngazi ya jamii.

Akisoma taarifa fupi Mwakilishi wa UN Women nchini Tanzania Hodan Addou ameeleza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuwawezesha wanawake kwenye nyanja mbalimbali ikiwepo kwenye uongozi ambapo wanawake wengi hivi sasa wanajitokeza kugombea nafasi mbalimbali hivo kuleta Maendeleo na usawa wa kijinsia

Hodan amesema kuwa Shirika hilo litaendelea kuwa mshirika wa karibu wa Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha kuwa wanawake na wasichana wanawezeshwa kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Nao Wanawake wajasiliamali wa soko la Machinga Complex wameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Finland pamoja na UN Woman Kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuwawezesha katika nyaja mbalimbali.

No comments:

Post a Comment