DIRA YA MAENDELEO 2050 KUKAMILIKA, SERIKALI YATAMANI UCHUMI WA TRILIONI MOJA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, June 19, 2025

DIRA YA MAENDELEO 2050 KUKAMILIKA, SERIKALI YATAMANI UCHUMI WA TRILIONI MOJA



Na Alex Sonna,Dodoma


Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais , Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida, amesema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho kukamilisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ambayo itakuwa mwongozo wa muda mrefu wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa miongo ijayo.

Akizungumza Juni 19, 2025, jijini Dodoma katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Dkt. Kida ameeleza kuwa rasimu ya Dira hiyo inatarajiwa kuwasilishwa bungeni tarehe 26 Juni 2025 na iwapo itaridhiwa na Bunge, itazinduliwa rasmi na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

“Kazi kubwa ya ofisi yetu kwa sasa ni kukamilisha maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050. Itakapopitishwa na Bunge, itakuwa dira rasmi ya nchi na baadaye kuzinduliwa na Mheshimiwa Rais Samia,” amesema Dkt. Kida.

Amefafanua kuwa pamoja na Dira hiyo, Serikali pia itatunga mpango wa muda mrefu utakaobainisha hatua mahsusi na mikakati ya kufikia malengo makuu ya Dira hiyo, ikiwemo kujenga uchumi wenye thamani ya takribani trilioni moja kwa kipindi hicho.

Dkt. Kida amebainisha kuwa Dira ya 2050 inalenga kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi, hususan wawekezaji wa ndani, katika kuongeza uzalishaji, ajira na mapato ya taifa.

Amesema kuwa mazingira ya uwekezaji yameboreshwa, huku Serikali ikizingatia vigezo vya kiwango cha mtaji, idadi ya ajira na mchango wa mwekezaji katika uchumi wa taifa bila kujali uraia wake.

“Tunataka kufikia uchumi wa mafanikio wa Trilioni moja,hatuwezi kufika huko bila sekta binafsi kushiriki kikamilifu ndiyo maana tunasisitiza kuwa wawekezaji wa ndani wapewe kipaumbele na waendelee kuwekewa mazingira rafiki ya kuwekeza,” ameeleza.

Akizungumzia ushiriki wa wananchi kwenye maonesho hayo, Dkt. Kida amesema kuwa zaidi ya wananchi 100 tayari wametembelea banda la ofisi yake, wakionesha kiu ya kuelewa majukumu mapya ya Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, hususan katika kuratibu miradi mikubwa ya kitaifa.

“Tunafurahi kuona mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi. Wanataka kufahamu kwa undani kazi za ofisi yetu, hususan kuhusu mipango ya muda mrefu ya maendeleo, kama vile mpango wa Dira ya 2050,” ameongeza.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kida alieleza kuwa ofisi hiyo imeboresha utoaji wa huduma kwa umma kupitia kliniki za papo kwa hapo, ambapo wananchi wanapata elimu na huduma moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wa mipango na uwekezaji waliopo katika viwanja vya maonesho.

Kwa ujumla, Dira ya 2050 inalenga kuweka Tanzania katika njia thabiti ya mafanikio ya muda mrefu, huku Serikali ikitoa wito kwa wadau wa sekta zote kuunga mkono juhudi hizo kwa vitendo.

No comments:

Post a Comment