DKT. NCHEMBA NA BALOZI WA NORWAY WAJADILI KUKUZA USHIRIKIANO WA KIUCHU NA KIJAMII - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, June 6, 2025

DKT. NCHEMBA NA BALOZI WA NORWAY WAJADILI KUKUZA USHIRIKIANO WA KIUCHU NA KIJAMII


Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwa na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mhe. Teni Tone Tennis, katika Ofisi za Hazina (Treasury Square), jijini Dodoma, baada ya kukutana na kufanya mazungunguzo ya namna ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Norway na Tanzania ambapo miongoni mwa maeneo yaliyojadiliwa ni kuimarisha sekta za kilimo, mabadiliko ya tabianchi, ukusanyanyaji wa mapato ya ndani, kusaidia makundi ya kijamii kupitia TASAF na kuimarisha biashara na uwekezaji nchini.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WF-Dodoma)


TANZANIA NA NORWAY KUIMARISHA USHIRIKIANO

Na Saidina Msangi,WF, Dodoma

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amesema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Norway umefanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ikiwemo miradi ya elimu, usambazaji wa umeme vijijini yenye thamani zaidi ya sh. bilioni 188.

Dkt. Nchemba alibainisha hayo Jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Norway nchini, Mhe. Teni Tone Tennis, ambapo pamoja na mambo mengine, walijadiliana namna ya kukuza maeneo mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo kilimo, mabadiliko ya tabianchi, kusaidia kaya masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF, na ukusanyaji wa mapato ya ndani ya nchi.

“Norway imekuwa mshirika wetu wa karibu katika kuhakikisha maendeleo endelevu ya kiuchumi nchini ikiwemo kuwezesha usambazaji wa umeme mkoani Lindi kupitia Wakala wa Nishati Vijijini wenye thamani ya bilioni 48.1’’, alisema Mhe. Nchemba.

Alisema kuwa Serikali ya Norway pia imetoa ufadhili wa kujiendeleza kielimu kwa wahandisi wanawake kwa kiasi cha sh. bilioni 4.68 ikiwa ni juhudi za kuleta usawa wa kijinsia nchini.

Dkt. Nchemba aliongeza kuwa mradi mwingine unaofadhiliwa na Norway ni Programu ya Usalama wa Jamii ya Kukuza Uzalishaji (PSSN II), tangu mwaka 2020 ambapo nchi hiyo imechangia kiasi cha shilingi bilioni 136.5.

‘’Baada ya mafanikio ya Mpango wa PSSN II unaotarajiwa kukamilika mwezi Septemba 2025, Serikali ya Tanzania inaandaa PSSN III ambao utazingatia kuisaidia jamii katika mazingira ya mabadiliko ya tabianchi na changamoto za kiuchumi, hivyo tunatamani Serikali ya Norway itaendelea kuunga mkono utekelezaji wa programu hii kwa manufaa ya wananchi wetu’’, alisema Dkt. Nchwemba.

Aliongeza kuwa tangu miaka ya 1990, Serikali ya Norway imekuwa ikiisaidia Tanzania kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ikiwemo utekelezaji wa Mpango wa Kisasa wa Kodi uliomalizika mwaka 2022 ambapo sasa, Serikali inasubiri ripoti rasmi ya Kikosi Kazi cha Rais kuhusu mageuzi ya kodi, kabla ya kuanza kutekeleza mapendekezo yake.

Aidha, Dk. Nchemba alisisitiza kuwa Tanzania inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Norway katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22–2025/26), hususan kwenye sekta za nishati, elimu, ukuaji wa uchumi, na mabadiliko ya tabianchi.

Aliongeza kuwa Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejizatiti kuendeleza ushirikiano wa karibu na Serikali ya Norway kwa ajili ya ustawi wa wananchi wa nchi hizo mbili.

Kwa upande wake Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mhe. Teni Tone Tennis, alisema kuwa nchi yake itaendeleza kushirikiana na Tanzania ili kuhakikisha kuwa nchi inafikia maendeleo ya kiuchumi na kijamii huku akipongeza hatua ya maendeleo iliyofikiwa na kuhimiza kuendeleza juhudi hizo katika ujenzi wa Tanzania mpya, yenye maendeleo jumuishi na endelevu.

Alipongeza mafanikio ya Serikali katika utekelezaji wa mradi wa treni ya mwendokasi (SGR) ambao ni nguzo muhimu ya kuimarisha usafirishaji wa bidhaa na kuunganisha nchi za ukanda wa Maziwa Makuu kiuchumi na kijamii na kuwa ni mfano wa kuigwa kwani umerahisisha shughuli za kiuchumi.

‘‘Ninapenda kutoa pongezi za dhati kwa hatua ya kuanza kusafirisha mizigo kupitia reli ya SGR, ni hatua muhimu si tu kwa Tanzania, bali kwa kanda nzima ya Afrika Mashariki. Kupitia hatua hii, Tanzania inaonesha uongozi wa mfano ambao mataifa ya jirani yanaweza kujifunza na kuiga’’, alisema Mhe. Tennis.

Alisema Tanzania inazidi kutambulika kimataifa kwa juhudi zake katika sekta ya usafiri na miundombinu ambapo mbali na maendeleo ya reli, imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi zenye thamani kubwa zikiwemo gesi asilia, ardhi yenye rutuba kwa kilimo, pamoja na madini ya kila aina.

Ushirikiano wa Tanzania na Norway umejikita katika nyanja za kiuchumi na kijamii hatua ambayo Norway imeahidi kuuendeleza kupitia uwekezaji wa mitaji na kukuza biashara kwa manufaa ya nchi hizo mbili.

No comments:

Post a Comment