DKT.BITEKO AZINDUA MKAKATI WA TAIFA WA MAWASILIANO WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, June 2, 2025

DKT.BITEKO AZINDUA MKAKATI WA TAIFA WA MAWASILIANO WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
(katikati) akizindua Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wa Nishati ya
Kupikia jijini Dodoma tarehe 2 Juni 2025. Kulia kwake ni Naibu Waziri
wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, kushoto ni Lamine Diallo ambaye ni
Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali watu kutoka Umoja wa Ulaya (EU).
Wengine katika picha ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi. Rosemary Senyamule
(wa tatu kushoto) ,Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge Nishati na
Madini Mhe. David Mathayo David (wa Pili kushoto), Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba (Wa pili kulia) na
Mshauri wa Rais katika Nishati Safi ya Kupikia na Maendeleo ya Jamii,
Angellah Kairuki


Na Mwandishi Wetu Dodoma


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amezindua Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia,

pamoja na Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji na Uelimishaji kuhusu
Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia lengo likiwa ni kuongeza uelewa wa
wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia na hivyo kuwezesha
asilimia 80 ya Watanzania kuhamia katika matumizi ya Nishati Safi ya
Kupikia ifikapo 2034.

Akizindua Mkakati huo wa Mawasiliano jijini Dodoma, Juni 2,2025, Dkt.
Biteko ameagiza kuwa mkakati huo usiishie kukaa kwenye makabati bali
utekelezwa katika ngazi zote za Serikali hadi ngazi ya mtaa bila
kusahau Sekta binafsi, wadau wa maendeleo pamoja na vyombo vya Habari
kuwa mstari wa mbele katika kuutekeleza.

Katika uzinduzi huo, Dkt. Biteko amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kuwa kinara namba moja wa matumizi ya Nishati safi ya
kupikia ndani na nje ya nchi ambapo kutoka azindue Mkakati wa Taifa wa
Matumizi ya Nishati safi ya kupikia (2024-2034) mnamo tarehe 08 Mei,
2024 matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia yameongezeka kutoka asilimia
6 hadi 16.

“ Katika kuthibitisha jinsi anavyolipa umuhimu suala hili la Nishati
Safi ya Kupikia, Mheshimiwa Rais pia ameunda Kitengo cha Nishati Safi
ya Kupikia ambacho kina jukumu maalumu la kusimamia ajenda ya nishati
safi ya kupikia na kwa kupitia kitengo hiki Serikali itaendelea na
shughuli mbalimbali ikiwemo kubuni na kusimamia miradi, pia kusimamia
kampeni zote za Kitaifa za uelimishaji na uhamasishaji wa nishati safi
ya kupikia.” Amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko ameeleza kuwa, matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia
inaendelea kuathiri afya na maisha ya watumiaji wengi hasa kina mama
na watoto chini ya umri wa miaka mitano ambapo taarifa zinaonesha
kuwa, watu bilioni 2.1 sawa na asilimia 24.7 ya Watu wote Duniani
hawana nishati safi ya kupikia ambapo kati yao watu Milioni 990 sawa
asilimia 47.1 ya wanaotumia nishati isiyo salama wanatoka barani
Afrika.

Ameeleza kuwa, Afrika inalazimika kufunga mkanda katika safari ndefu
ya kuelekea kwenye matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambapo kwa
upande wa Tanzania amesema kuwa kila Taasisi inapaswa kutambua na
kutekeleza jukumu lake kikamilifu.

Dkt. Biteko amewasisitiza Wadau wote wanaohusika na Nishati Safi ya
Kupikia kuhakikisha kuwa wanandaa na kutekeleza Kampeni zinazolenga
makundi maalum katika jamii, kukuza uelewa wa umma kuhusu njia za
ufadhili na gharama nafuu, kuhakikisha ujumbe thabiti wenye kueleweka
miongoni unafika kwa wadau wote na kuendeleza na kuimarisha njia za
mawasiliano za kuaminika.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameiagiza Wizara ya Nishati kupitia
Kitengo cha Tathmini na Ufuatiliaji inafanya tathmini katika kila robo
mwaka ili kuweza kujipima juu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa
Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule
amempongeza Rais, Dkt. Samia kwa kuendelea kuonesha kuwa nishati safi
ya kupikia si suala la maneno bali ni vitendo na ndio maana
anatambulika duniani kama kinara wa nishati safi ya kupikia.

Amesema kuwa suala la Nishati Safi ya Kupikia ni kipaumbele cha Mkoa
wa Dodoma ambapo juhudi mbalimbali zinachukuliwa kuhamasisha
matumizi ya nishati safi ya kupikia akitoa mfano kuwa kwa Mkoa wa
Dodoma kwa sasa tayari magereza 9 yanatumia nishati safi ya kupikia,
shule za VETA 3 na shule 9 za bweni huku kazi ya uhamasishaji
ikiendelea.

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema katika kipindi
cha miaka minne sekta ya Nishati imekuwa mashuhuri kwa masuala
mbalimbali kubwa likiwa ni nishati safi ya kupikia na kueleza kuwa
nguvu ya ushawishi ya Rais, Dkt.Samia imefanya ajenda ya nishati safi
ya kupikia kukubalika ndani na nje ya nchi na hivyo kutoa hakikisho la
usalama wa afya na mazingira pia.

Ameongeza kuwa Mkakati wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia
uliozinduliwa utaongeza kasi za programu za nishati safi ya kupikia na
kuleta mapinduzi ya kuhama kutoka matumizi ya nishati isiyo safi ya
kupikia kwenda kwenye nishati safi ya kupikia.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema
kuzinduliwa kwa Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya
Kupikia ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa
Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Ameeleza kuwa Mkakati huo umezinduliwa na Wizara ya Wizara ya Nishati
na kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Mitaji la Umoja wa
Mataifa (UNCDF) chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) ambapo
Mkakati huo unaongozwa na kaulimbiu ya kitaifa isemayo “Nishati Safi
ya Kupikia, Okoa Maisha na Mazingira”,

Amesema lengo kuu la mkakati ni kuongeza uelewa wa wananchi na taasisi
kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na malengo
mengine mahususi ni kuandaa na kutekeleza kampeni maalum za
uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, kuhakikisha
ujumbe wenye lengo la pamoja unafika kwa wadau wote pamoja na
kuendeleza na kuimarisha njia za mawasiliano.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini,
Mhe. David Mathayo amempongeza Rais, Dkt. Samia kwa kuanzisha gurudumu
la Nishati Safi ya Kupikia, pia amempongeza Dkt. Biteko kwa jinsi
anavyoongoza Wizara na kutoa ushirikiano kwa kamati hiyo.

Aidha, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Rodney Thadeus amesema kuwa
Wizara hiyo itahakikisha mkakati wa mawasiliano uliozinduliwa
unatekelezwa kwa mafanikio kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati
pamoja na wadau wengine vikiwemo vyombo vya Habari.

Vilevile, Mshauri wa Rais ( Nishati Safi ya Kupikia na Maendeleo ya
Jamii) Angellah Kairuki amepongeza juhudi za serikali katika
kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia huku kielelezo mojawapo
kikiwa ni uzinduzi wa mkakati wa mawasiliano ambao ni muhimu katika
kufikisha ujumbe kwa umma kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safibya kupikia.

Naye, Lamine Diallo, Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali kutoka Umoja wa
Ulaya ( EU), ameipongeza Wizara ya Nishati kwa tukio hilo muhimu la
kuzindua Mkakati wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia na kusema
kuwa inaonesha kwa vitendo juhudi za Serikali katika kuboresha maisha
ya wananchi kupitia Nishati Safi ya Kupikia.

No comments:

Post a Comment