
Na Bahati Mollel, Dodoma
Ujenzi wa jengo la ofisi za Makao Makuu ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) linalojengwa maeneo ya Jedengwa jijini Dodoma limefikia asilimia 68 ili kukamilika.
Mhandisi Fredy Kambi anayesimamia ujenzi huo, amesema ofisi hizo zitakuwa kwenye maghorofa mawili pacha yenye ghorofa saba kila mmoja, ambazo zitatumika na Kurugenzi na Idara mbalimbali zilizopo kwenye taasisi hiyo.

Mhandisi Kambi amesema ujenzi huo ulianza tarehe 01 April, 2024 na unatekelezwa kwa miezi 14 na sasa mkandarasi ameongezewa siku 167 na unatarajiwa kukamilika tarehe 15 Septemba, 2025, ambapo mbali na majengo pacha ya ofisi pia kumechimbwa visima vya maji safi, kusimikwa kwa tanki kubwa la maji lenye ujazo wa lita milioni moja, na kutakuwa na uvunaji wa maji ya mvua kwa ajili ya matumizi mbalimbali, na kumejengwa ukuta wa usalama.
Halikadhalika, Mhandisi Kambi amesema majengo hayo pacha yatakuwa na kumbi za kisasa za mikutano, majenereta makubwa ya umeme wa dharura yenye Kv 23, na kutasimikwa mfumo wa umeme jua, ambao utatumika endapo umeme wa shirika la umeme Tanzania (TANESCO) utakatika; pia kutakuwa na barabara za kuingia jengoni na maegesho ya magari takribani 150.
Amesema mradi huu upo chini ya usimamizi wa Wakala ya Majengo Tanzania (TBA) na mkandarasi ni CRJ East Afrika, ambapo pia kunajengwa maabara kubwa ya Kimataifa itakayokuwa ikitumiwa na watanzania na nchi za nje kupima malighafi wanazokwenda kuzitumia kwenye majenzi mbalimbali pamoja na kufanya tafiti, pia kumejengwa maghala mawili.
“Tunategemea ndani ya kipindi kilichobaki kwa muda uliopangwa kunauwezekano wa kukamilika kwa majengo haya, na yakaanza kutumika, kutokana na mkandarasi kampuni ya CRJ kutoka China kushirikiana na wataalam wa ndani,” amesisitiza Mhandisi. Kambi.
Ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyopo chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha kutekeleza mradi huu kwa ufanisi mkubwa.





No comments:
Post a Comment