RADIO JAMII WANOLEWA UANDISHI WA HABARI ZA USTAWI WA WATOTO NA VIJANA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, June 13, 2025

RADIO JAMII WANOLEWA UANDISHI WA HABARI ZA USTAWI WA WATOTO NA VIJANA.



Waandaji Vipindi na watangazaji kutoka Radio Jamii za Tanzania bara na Visiwani wamepewa mafunzo ya namna ya kuandika habari za ustawi wa vijana na watoto, kupinga ukatili, afya ya uzazi na kupambana na mimba za na ndoa utotoni ili kuelimisha na kuchukua hatua za kupinga vitendo hivyo.

Mafunzo hayo ya Siku nne (4) yaliyofanyika mjini Morogoro kuanzia tarehe 9 hadi 12 Juni 2025 yameandaliwa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Akizungumza katika Mafunzo hayo Mratibu wa mafunzo kutoka UNESCO Mathias Luhanya amesema wanahabari ni nyenzo muhimu katika kuleta mabadiliko chanya kwa jamii, hivyo wanawajibu wa kuandika na kuandaa vipindi vya elimu ili jamii iweze kuelewa na kuchukua hatua kuzuia vitendo vinavyoathiri ustawi wa watoto na vijana.

"Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuandaa vipindi vya kijamii vinavyoelimisha kuhusu ustawi wa afya ya vijana, athari za mimba na ndoa za utotoni, kupinga ukatili wa kijinsia na ujumuishaji watu wenye mahitaji maalum.

"Kupitia mafunzo haya ni wajibu wenu kuandaa vipindi shirikishi vya kijamii ili kuangazia changamoto zao na wao wenyewe kuwa sehemu ya kuleta mabadiliko na kwa njia hiyo mtasaidia kuleta ustawi wa vijana kwa maendeleo ya Taifa" amesema Mathias.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Rehema Kombe amewaomba waandishi hao kuendelea kushirikiana na Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii katika maeneo yao ili kusaidia kutoa elimu kwa jamii kuhusu Ustawi wa vijana na watoto.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikali Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Raymond Mushumbusi amesema wanahabari wanapaswa kusoma kwa kina miongozo, mipango, mikakati, kanuni na sheria mbalimbali zinazohusu watoto na vijana ili kutoa taarifa sahihi kuhusu kundi hilo pale wanapotengeneza na kurusha vipindi vyao.

Naye Mshiriki wa mafunzo hayo Amua Akaro ameeleza kwamba mafunzo hayo ni chachu kwa wanahabari na yatasaidia kuandaa vipindi bora vinavyogusa afya na ustawi wa watoto na jamii kwa ujumla.





No comments:

Post a Comment