Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema utekelezaji wa miradi yote ya maji imelenga kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira, lakini pia ni muhimu kulinda mazingira ya Ziwa Victoria ambalo ni muhimu sana kwa maisha na maendeleo ya kibiashara katika Jiji la Mwanza na maeneo jirani.
Rais Dkt. Samia ametoa agizo hilo mara baada ya kuzindua rasmi Mradi wa Maji Butimba, wenye thamani ya Shilingi Bilioni 71.6, akisema kuwa mradi huo utaboresha kwa kiwango kikubwa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa wakazi wa Mwanza na maeneo jirani.
“Maziwa Makuu likiwemo Ziwa Victoria ni vyanzo vya uhakika vya maji kwa matumizi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii, hivyo niwakumbushe kuwa suala la uhifadhi wa mazingira ikiwemo kudhibiti kuenea kwa magugu maji katika Ziwa Victoria ni msingi wa uendelevu wa upatikanaji wa maji, kuwezesha shughuli mbalimbali za maendeleo kama vile kilimo, viwanda, ufugaji, uvuvi, utalii na usafiri kwa njia ya maji,” Rais Samia amesema.
“Kwa muktadha huo, Naagiza juhudi za kuhifadhi mazingira ziendelee kufanyika kikamilifu kwa kushirikisha sekta zote,” Rais Samia ameagiza
Aidha, Rais Dkt. Samia amefurahishwa na mradi kuhusisha ujenzi wa vyoo vya kisasa vya umma vipatavyo 107 katika mashule, zahanati na masoko katika Wilaya za Nyamagana na Ilemela. Akisema kuwa ni dhahiri kuwa programu hii ya LVWATSAN imegusa maisha ya kila siku ya wananchi wa Jiji la Mwanza.
Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa Mradi huu umetekelezwa kupitia Programu ya Lake Victoria Water and Sanitation (LVWATSAN) kwa ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank - EIB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (Agence Française de Développement - AFD). Akitoa shukrani kwa Washirika na Wadau wa Maendeleo kwa ushirikiano wao na Serikali katika kuleta maendeleo.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa kupitia programu ya LVWATSAN awamu ya kwanza, miradi ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya namna hii imetekelezwa na kukamilika katika Miji ya Magu na Misungwi Mkoani Mwanza, pamoja na Mji wa Lamadi uliopo Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu ambao ameuzindua siku ya jana.
Awali, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema kuwa kabla ya mradi huu, Jiji la Mwanza lilikuwa likitegemea chanzo cha Capripoint chenye uwezo wa kuzalisha lita 90,000,000 kwa siku wakati mahitaji yalikuwa ni lita 188,000,000. “Kupitia mradi wa Butimba, uzalishaji umeongezeka hadi kufikia lita 138,000,000 kwa siku, hatua ambayo imepunguza migao ya maji na kuongeza muda wa upatikanaji wa huduma,” Waziri Aweso amesema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amefafanua kuwa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa Jiji la Mwanza mwaka 2021 ilikuwa wastani asilimia 63.15, hivi sasa upatikanaji wa maji umeongezeka na kufikia wastani wa asilimia 87, ongezeko hili limechangiwa na kukamilika kwa miradi ya usambazaji maji ukiwemo ujenzi wa chanzo cha Butimba. Aidha, amesisitiza matarajio ya Wizara ya Maji ni kufikia wastani wa asilimia 98 mwezi Desemba 2026 baada ya mradi wa usambazaji kukamilika.
Maeneo yanayonufaika na mradi huu ni pamoja na Nyegezi, Mkolani, Buhongwa, Nyamazobe, Nyahingi, Buganda, Luchelele, Lwanhima, Sahwa, Fumagila, Kishiri na Igoma katika Jiji la Mwanza, pamoja na maeneo ya Kisesa, Bujora na Kanyama katika Wilaya ya Magu.
No comments:
Post a Comment