Katika kuhakikisha usimamizi madhubuti wa Sekta ya Huduma Ndogo za Fedha, Serikali imewaagiza waratibu wa biashara ya huduma ndogo za fedha kote nchini kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa Sera na Sheria za Huduma Ndogo za Fedha katika maeneo wanayoyasimamia ili kuwabaini na kuwachukulia hatua watoa huduma wanaotoa huduma kinyume na utaratibu uliowekwa.
Agizo hilo limetolewa na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Fedha, Wizara ya Fedha Bi. Dionesia Mjema, wakati akifunga mafunzo ya kitaalamu kwa watoa huduma ndogo za fedha kutoka katika ngazi za mikoa, wilaya na halmashauri, yaliyolenga kuwaongezea ujuzi wa kiutendaji katika kutambua changamoto, kushughulikia ukiukwaji wa sheria na kuwajengea uwezo wa kusimamia kwa ufanisi huduma hizo.
“Ni muhimu kila mmoja wetu awe mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha inatekelezwa ipasavyo, na wale wanaokiuka Sheria hiyo wanachukuliwa hatua stahiki,” alisema Bi. Mjema.
Alisisitiza kuwa utekelezaji wa Sheria si chaguo bali ni wajibu wa kila mtoa huduma na msimamizi wa sekta hii, kwa kuwa utekelezaji huo ndio msingi wa kuhakikisha uwajibikaji, uadilifu, na uendelevu wa huduma ndogo za fedha katika kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Aidha, aliwasisitiza kujenga mazoea ya kuandaa na kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa Sheria hizo kila baada ya miezi mitatu, kwa mujibu wa miongozo, kwa kuwa taarifa hizo ni nyenzo muhimu katika kutathmini maendeleo, changamoto na mafanikio ya utekelezaji wa sheria katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Bi. Mjema, aliwasihi waratibu hao kushirikiana kwa karibu na maafisa ushirika, wahamasishaji, wasajili, pamoja na maafisa maendeleo ya jamii, ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wa Sera na Sheria za Huduma Ndogo za Fedha unafanyika kwa ufanisi.
“Ushirikiano huo unatarajiwa kujenga mfumo madhubuti na endelevu wa huduma ndogo za fedha, unaolenga kuwafikia wananchi wa kipato cha chini kwa kutumia mbinu bora, salama na zenye ufanisi, ili kuchochea ustawi wa kiuchumi na kuchangia maendeleo jumuishi ya taifa zima”alisema Bi. Mjema.
Kwa upande wake, Mratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha mkoani Mbeya, Bi. Sebastiana Mwapinga, ambaye alikuwa miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo, alisema kuwa mafunzo hayo yamekuwa kichocheo muhimu cha mabadiliko chanya, na kwamba wataendelea kuboresha utendaji wao hususan katika maeneo yaliyokuwa na changamoto hapo awali, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kifedha zitakazowawezesha kuinua hali zao za kiuchumi.
Naye, mmoja wa wahamasishaji, Bi. Teodomila Mwenda, amesema kuwa hatua ya Serikali kuwapatia mafunzo na kuwajengea uwezo wa kitaalamu siyo tu imedhihirisha dhamira yake ya dhati ya kuimarisha sekta hiyo, bali pia imeongeza ari na motisha kwao kuendelea kutoa elimu kwa ufanisi zaidi.
Katika mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha, taasisi mbalimbali zilipata fursa ya kutoa elimu kuhusu huduma za uwekezaji wanazotoa ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji UTT- AMIS, Mfuko wa SELF pamoja Watumishi Housing Investment ambazo ni muhimu kwa wananchi kuzifahamu na kuzitumia ipasavyo ili kuongeza kipato chao na kuboresha maisha yao ya kiuchumi.
Jumla ya waratibu 130 wa huduma ndogo za fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri wamepatiwa mafunzo ya kitaalamu katika maeneo mbalimbali, yaliyolenga kuwaimarisha katika kusimamia na kufuatilia kwa ufanisi utoaji wa huduma ndogo za fedha katika ngazi za watoa huduma.
No comments:
Post a Comment