
Waziri wa Fedha, Mhe Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akimkabidhi zawadi yenye bidhaa za Tanzania, Balozi wa Canada nchini Tanzania, Mhe. Emilly Burns, baada ya kuhitimisha mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Waziri wa Fedha, Treasury Square jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WF-Dodoma)
Na Saidina Msangi, WF, Dodoma
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amesema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Canada umefanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ikiwemo miradi mipya miwili inayotekelezwa hivi sasa katika sekta za afya na elimu nchini yenye thamani zaidi ya sh. bilioni 248.5.
Dkt. Nchemba alibainisha hayo Jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Canada nchini, Mhe. Emilly Burns, ambapo pamoja na mambo mengine, walijadiliana namna ya kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kijamii pamoja na kuimarisha biashara kati ya Tanzania na Canada.
‘‘Tayari tuna miradi miwili ya ushirikiano na utekelezaji wake unaendelea katika sekta ya elimu yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 102.9 na sekta ya afya zaidi ya sh. bilioni 145.6, ambapo nusu ya fedha hizo zimeshapokelewa na utekelezaji wa miradi unaendelea’’, alisema Dkt. Nchemba.
Aidha, Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania imefungua milango kwa Kampuni ya FinDev inayomilikiwa na Serikali ya Canada kuja kuwekeza fedha katika Benki ya CRDB na TCB za hapa Tanzania kwa ajili ya kuwakopesha na kukuza mitaji ya wajasiliamali wadogo.
Alisema Serikali iko tayari kufufua ushirikiano uliokuwepo kwenye masuala ya kodi kati ya Tanzania na Canada na kueleza kuwa Serikali inatoa mazingira mazuri ya nafuu ya kodi kwa kampuni ama taasisi za nje zinazotoa fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta ya fedha kwa riba nafuu ili kuwawezesha wakopaji kwenye taasisi hizo kupata mikopo kwa riba nafuu zaidi.
‘‘Hili ni jambo jema, timu zetu za wataalamu zitaendelea kulifanyia kazi ili tuweze kuhakikisha kwamba maeneo haya ambayo yanapunguza kasi ya kushirikiana katika maeneo ya fedha yarekebishwe’’, alifafanua Dkt. Nchemba.
Aliongeza kuwa kwenye masuala ya kikodi, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliunda tume ambayo inaangalia upya mifumo ya kikodi pamoja na viwango vyake ambapo tayari imeshafanyia kazi maoni ya wadau kwa kiwango kikubwa.
‘‘Tunaamini kazi hiyo itakapokuwa imekamilika tutaboresha mifumo yetu kama nchi, lakini tutaweza kuvutia zaidi uwekezaji na mazingira bora ya kufanyia biashara ndani ya nchi yetu’’, aliongeza Mhe. Dkt. Nchemba.
Kwa upande wake Balozi wa Canada nchini Tanzania, Mhe. Emilly Burns, alisema kuwa Canada inathamini ushirikiano na Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo nchi hiyo inatoa kiasi cha dola za Canada milioni 141 kwa mwaka kutekeleza miradi katika sekta za elimu, afya na uendelezaji uchumi.
Alisema kufanikiwa kwa utekelezaji wa miradi hiyo kunatokana na ushirikiano mzuri ambao Tanzania unautoa kwa taasisi za Canada zinazofanya kazi nchini.
Aliipongeza Tanzania kwa kusimamia vizuri masuala ya Uchumi na kwamba Taasisi mbalimbali za kimataifa zikiwemo za fedha kama Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa, limekuwa likitoa mfano wa Tanzania kama nchi inayofanya vizuri zaidi katika usimamizi wa sera za fedha na Uchumi.
‘‘Nimewahi kufanyakazi nchini Zambia, na wakati ule tulikuwa na watu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa -IMF, ambao walikuwa wanaizungumzia Tanzania kuwa nchi ya mfano katika usimamizi wa Uchumi jambo ambalo ni kweli kabisa, ninawapongeza sana’’ alisema Mhe. Burns.
Ushirikiano wa Tanzania na Canada umetimiza miaka 60 hivi sasa na uhusiano huo umejikita katika Nyanja za kiuchumi na kijamii hatua ambayo Canada imeahidi kuuendeleza kupitia uwekezaji wa mitaji na kukuza biashara kwa manufaa yan chi hizo mbili.
No comments:
Post a Comment