
Dodoma, Juni 16, 2025
Maelfu ya wananchi kutoka Mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani wamejitokeza kwa wingi katika viwanja vya Chinangali kushiriki Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, huku wengi wakivutiwa na Banda la Tume ya Madini ambalo limekuwa kitovu cha elimu na maarifa kuhusu Sekta ya Madini.
Banda hilo limekuwa kivutio kikubwa kutokana na utoaji wa elimu ya kina kuhusu aina mbalimbali za madini yanayopatikana nchini, taratibu za upatikanaji wa leseni za utafiti, uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini pamoja na fursa za kiuchumi zinazopatikana kupitia sekta hiyo.
Wananchi wa rika zote wameonekana kuwa na shauku kubwa ya kupata uelewa kuhusu namna bora ya kushiriki kwenye shughuli za madini kwa njia salama, endelevu na zenye tija kwao binafsi na kwa taifa.
Afisa kutoka Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira kutoka Tume ya Madini, Ashen Mwambage ametoa elimu kwa wananchi kwa umahiri mkubwa, akielezea kwa kina umuhimu wa kulinda mazingira wakati wa shughuli za madini na namna ya kuzingatia sheria na taratibu ili kunufaika ipasavyo.
“Tunahamasisha wananchi kutumia fursa zilizopo katika Sekta ya Madini kwa kuzingatia kanuni za usalama na utunzaji wa mazingira. Sekta hii ni mhimili muhimu wa uchumi wetu, na kila Mtanzania ana nafasi ya kunufaika nayo,” ameeleza Mwambage
Aidha, wananchi wamepongeza juhudi za Tume ya Madini kwa kupeleka huduma karibu na wananchi kupitia maonesho hayo, wakisema elimu waliyoipata itawawezesha kufanya maamuzi sahihi kuhusu ushiriki wao katika sekta ya madini.
Tume ya Madini itaendelea kutoa elimu kwa wananchi katika kipindi chote cha maadhimisho, huku ikisisitiza ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya sekta hiyo yenye mchango mkubwa katika Pato la Taifa.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa Mwaka huu inayotarajiwa kumalizika Juni 23, 2025 ni _”Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidijiti ili Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji.



No comments:
Post a Comment