WAZIRI JAFO:SERIKALI ITAENDELEA KULINDA BIASHARA ZA WAZAWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, June 6, 2025

WAZIRI JAFO:SERIKALI ITAENDELEA KULINDA BIASHARA ZA WAZAWA



Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo,akziungumza leo Juni 6, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akipokea Taarifa ya Timu maalum ya Ukaguzi wa Biashara zinazomilikiwa na wageni. Katika Soko la Kariakoo.

......

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, amesema Serikali inaangalia uwezekano wa kupeleka hati ya dharura bungeni ili kuwezesha baadhi ya vifungu vya sheria vinavyolenga kulinda biashara za wazawa kuingizwa kwenye Muswada wa Sheria ya Fedha (Finance Bill) wa mwaka huu.

Dkt. Jafo amesema hayo Juni 6, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akipokea Taarifa ya Timu maalum ya Ukaguzi wa Biashara zinazomilikiwa na wageni. Katika Soko la Kariakoo.

Aidha, amesema Serikali itahihikisha mapendekezo ya Timu hiyo yanafanyiwa kazi ili kuhakikisha kuwa fursa za kiuchumi na kibiashara zinazalishwa na kusalia mikononi mwa Watanzania.

"Lengo ni kuhakikisha fursa za wazawa zinabaki kwa wazawa. Nimepokea taarifa ya timu iliyokuwa Morogoro iliyofanya kazi ya kubaini maeneo ya kisheria yanayohitaji maboresho ili kuainisha wazi ni maeneo gani ya biashara yanapaswa kuwa kwa wazawa na yapi yanaweza kufanywa na wageni," alisema Dkt Jafo.

Amesema tayari timu hiyo imekamilisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria mbalimbali, na kwamba wafanyabiashara nchini walishirikishwa kikamilifu katika kutoa maoni yao kwa wataalamu waliokuwa wakifanya kazi hiyo.

"Baadhi ya mapendekezo ya Timu Hiyo ni pamoja na kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Usajili wa Kampuni, Sura ya 212 ya mwaka 2002, Sheria ya Leseni no 25 ya 1972 na Sheria ya Uhamiaji sura ya 54 na marekebisho ya mwaka 2026 pamoja na Sheria ya Uwekezaji ambazo kwa sasa zimekuwa zikitumiwa kama mianya ya kuingiza wageni kwenye maeneo yaliyopaswa kutengwa kwa wazawa," alifafanua.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kufanya kazi ya kisheria kwa mujibu wa mapendekezo ya Timu na kwamba kama Haru ya dharura itapata kibali, vifungu hivyo vitaingizwa moja kwa moja kwenye Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka huu.

Hata hivyo, iwapo hati hiyo haitapata kibali, Serikali itahakikisha vifungu hivyo vinapelekwa kama mswada maalum au vinajadiliwa katika mabunge yajayo.

“Tunalenga kuhakikisha tunapata sheria madhubuti ambayo itaondoa mianya inayotumiwa na baadhi ya watu kujinufaisha kwa njia isiyo halali. Tukishindwa kupata fursa sasa, tutahakikisha baadhi ya vifungu hivyo vinaingizwa kwenye muswada wa fedha kwa mujibu wa taratibu nyingine,” alieleza Waziri.

Ameongeza kuwa hatua hii inalenga kulinda biashara zinazofanywa na Watanzania na kuweka msingi imara wa kisheria kwa maendeleo ya muda mrefu.

“Kuna biashara fulani ambazo tunapendekeza zifanywe na Watanzania tu kwa kuzingatia msingi wa ulinzi wa fursa za ndani. Hili linafanywa kwa hatua ya awali huku tukisubiri hatua nyingine kuendelea kujadiliwa kwenye vikao vya Bunge vijavyo,” alisema.

Waziri Jafo amesema matarajio ni kuwa ndani ya wiki tatu zijazo, Serikali itakuwa imepata mwelekeo sahihi kuhusu namna ya kusonga mbele na utekelezaji wa mapendekezo hayo.

"Tunataka Watanzania waendelee kunufaika na rasilimali zao kama ilivyo kwa mataifa mengine yanavyowalinda wananchi wao," alihitimisha.

Akiwasilisha ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Timu Bw Thabit Mussa alisema lengo la kamati ilikuwa kuangalia wafanyabiashara wa eneo la kariakoo wanafuata sheria, kanuni na taratibu za utoaji vibali na leseni katika ufanyaji biashara.

“Timu ilikagua biashara 108 ambazo zilibaini mapungufu mbalimbali ikiwa ni pamoja na baadhi ya biashara kutokuwa na leseni, biashara bandia, wapo walioshindwa kufika ofisi za TRA kukaguliwa na wengine walifutiwa vibali vya kufanya kazi nchini,” alisema Bw Massa.

Hata hivyo Massa alisema katika zoezi hilo waliweza kukusanya mapato ya shilingi milioni 393, 224,787/-

No comments:

Post a Comment