
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa George Boniface Simbachawene, amepongeza kazi bora ya ujenzi inayotekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), akieleza kuridhishwa na ubunifu na ubora wa majengo yanayojengwa na wakala huo.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika Banda la TBA kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma, Waziri Simbachawene amesema, “TBA mnafanya kazi nzuri katika ujenzi wa majengo ya Serikali. Hata jengo la Wizara ya Utumishi mmejenga ninyi, ni jengo zuri na linavutia. Hongereni sana.”
Aidha, Waziri Simbachawene amezihimiza taasisi zote za Serikali, ikiwemo TBA, kuendelea kutekeleza miradi ya umma kwa weledi na ufanisi ili kufanikisha malengo ya Serikali katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
TBA ni miongoni mwa taasisi za umma zinazoshiriki katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu, ambayo yamebeba kaulimbiu isemayo: “Himiza matumizi ya mifumo ya kidijiti ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na kuchagiza uwajibikaji.”
Maonesho hayo yameanza rasmi siku ya Jumatatu Juni 16, 2025, na yanatarajiwa kufungwa Juni 23, 2025, yakihusisha taasisi mbalimbali za umma zinazowasilisha huduma na mafanikio yao kwa umma.
Katika banda la TBA, wananchi wanapata fursa ya kujifunza kuhusu miradi ya ujenzi inayotekelezwa na wakala huo, pamoja na kuona mchango wake wa maendeleo kwenye Sekta ya ujenzi.



No comments:
Post a Comment