ADEM YATOA MAFUNZO YA UONGOZI KWA MAAFISA ELIMU KATA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, July 10, 2025

ADEM YATOA MAFUNZO YA UONGOZI KWA MAAFISA ELIMU KATA


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Wakala wa Maendeleo ya Usimamizi wa Elimu (ADEM), imeendelea kutoa mafunzo endelevu kwa viongozi wa elimu katika ngazi mbalimbali nchini, ili kuboresha usimamizi na uendeshaji wa shule kwa lengo la kuinua viwango bora vya elimu.

Akizungumza Julai 9, 2025 wakati wa Uzinduzi wa mafunzo ya Uongozi wa Usimamizi wa Shule na Utawala Bora wa Elimu kwa Maafisa Elimu Kata, Katibu Mkuu Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, amesisitiza umuhimu wa ADEM kuendelea kutoa ushauri wa kitaalamu, kufanya tafiti, na kukuza ufanisi kwa njia endelevu.

Prof. Nombo amesema kuwa maboresho yanayoendelea kufanyika katika sekta ya elimu yanapaswa kusimamiwa kwa weledi na viongozi wa elimu kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ambao ndio wasimamizi wa utekelezaji wa utoaji elimu.

Katibu Mkuu huyo ameishukuru Benki ya Dunia kupitia Mradi wa BOOST, ambayo umewezesha upatikanaji wa moduli muhimu kama vile Kitabu cha Utawala Bora wa Elimu na Mwongozo wa Mwezeshaji ambazo zimebuniwa kusaidia viongozi wa elimu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, sambamba na vifaa vya kujifunzia na kufundishia.

"Mafunzo haya si tu ya kujifunza, bali ya kuleta mabadiliko ya kweli. Tathmini itafanywa kwa kuzingatia viashiria vya ufanisi vilivyobainishwa. Tukishindwa kuleta mabadiliko chanya, tutakuwa tumepoteza rasilimali na muda,” aliasa Prof. Nombo.

Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid Maulid, amebainisha kuwa awamu ya kwanza ya mafunzo inahusisha Maafisa Elimu Kata zaidi ya 1,000 kutoka mikoa 12, huku awamu ya pili ikitarajiwa kuhusisha mikoa 14, na kufanya idadi ya washiriki kufikia zaidi ya 3,000.

Mafunzo hayo yanatajwa kuwa chachu ya mabadiliko katika kuandaa viongozi wenye uwezo wa kusimamia kwa weledi na kutoa elimu bora inayotakiwa katika karne ya 21.



No comments:

Post a Comment