
Tarehe 15.07.2025 katika Mahakama ya Wilaya ya Kakonko limefunguliwa Shauri la Uhujumu Uchumi lililosajiliwa kwa nambari ECC.17155/2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mh. Maila Makonya (SRM).
Washtakiwa hao ni Bw. Denis Simon Manji (36) ambaye ni Fundi sanifu maji RUWASA Wilaya ya Kakonko na Mshtakiwa wa pili ni Bw. Benjamin Mjuni Brighton (38) ambaye ni Meneja RUWASA Wilaya ya Kakonko.
Washtakiwa hao wanashtakiwa kwa Makosa ya Matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri kinyume na kifungu cha 22, Ubadhirifu na ufujaji kinyume na kifungu cha 28 (1), vyote vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, vikisomwa pamoja na Aya ya 21 ya Jedwali la kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupanga Sura ya 200 marejeo ya mwaka 2022 na kosa la kughushi kinyume na kifungu cha 333, 335(a) (d )(i)(ii) na 337 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16 kama ilivyorejewa 2022. Kwamba washtakiwa Bw. Denis Simon Manji (36) na Bw. Benjamin Mjuni Brighton (38) wamefanya ubadhirifu wa fedha kiasi cha Tshs. 9,970,000 zilizotolewa kwa ajili ya kuwezesha shughuli za maadhimisho ya wiki ya Maji wilaya ya Kakonko kwa mwaka 2023.
Washtakiwa hao kwa nia ovu, walighushi Saini za Wajumbe wa Kamati ya Usalama Wilaya ya Kakonko, Viongozi wa chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kakonko na wajumbe kutoka ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, kuonesha kuwa walishiriki maadhimisho ya kilele cha wiki ya maji yaliyofanyika mnamo mwezi Machi, 2023 na kulipwa posho za ushiriki wakati si kweli.
Washtakiwa hao walikana mashtaka yote waliyosomewa na walikidhi masharti ya dhamana hivyo wako nje kwa dhamana hadi tarehe 29.07.2025 shauri litakapoitwa tena mahakamani.
Shauri hili linaendeshwa na wakili wa Serikali kutoka TAKUKURU Bw. Augustino Lohay
TAKUKURU KAKONKO, Julai 16, 2025
No comments:
Post a Comment