
Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Mhe. Hamad Khamis Hamad, leo tarehe 07 Julai 2025 amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Margarida Adamugu Talapa, Rais wa Bunge la Jamhuri ya Msumbiji, katika Ofisi za Bunge hilo Jijini Maputo.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Talapa alimpongeza Balozi Hamad kwa kuteuliwa kuiwakilisha Tanzania nchini Msumbiji, huku akimhakikishia ushirikiano wa karibu katika utekelezaji wa majukumu yake ya kibalozi. Alisisitiza kuwa Msumbiji inathamini uhusiano wa kihistoria kati ya nchi hizo mbili, hususan mchango mkubwa wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa taifa hilo pamoja na msaada wake katika jitihada za kurejesha amani Kaskazini mwa Msumbiji.
Kwa upande wake, Balozi Hamad alimshukuru Rais wa Bunge kwa mapokezi mazuri na kwa kukubali kukutana naye. Alieleza dhamira ya Tanzania kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na wa kibunge kati ya nchi hizo mbili, akisisitiza umuhimu wa Mabunge ya Tanzania na Msumbiji kuimarisha mahusiano na kubadilishana uzoefu, hasa baada ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Tanzania mwezi Oktoba 2025.
Aidha, Balozi Hamad alieleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wananchi wa Msumbiji katika nyanja mbalimbali, ikiwemo juhudi za kuhakikisha amani ya kudumu Kaskazini mwa Msumbiji, ambapo Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania yanaendelea kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya vikundi vya kigaidi.
Imetolewa na:
Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Maputo, Msumbiji



No comments:
Post a Comment