MAJALIWA AITAKA TRA KUENDELEA KUONGEZA UFANISI UKUSANYAJI KODI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, July 8, 2025

MAJALIWA AITAKA TRA KUENDELEA KUONGEZA UFANISI UKUSANYAJI KODI


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuongeza usimamizi wa ukusanyaji wa kodi kwa wafanyabiashara ikiwemo wa mataifa ya nje walioamua kuja kufanya shughuli zao nchini.
 
Amesema kuwa TRA inapaswa kuongeza ufanisi zaidi kwenye kuwasimamia wafanyabiashara wote kuhakikisha wanatambua sheria za ulipaji kodi pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakiki utekelezaji wake.
 
Ametoa agizo hilo leo (Jumanne Julai 08, 2025) alipofungua kikao kazi cha Viongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kituo cha Mikutano cha Arusha (IACC).
 
“Nendeni mkachunguze hawa wanaokuja kufanya biashara nchini, kama wanaondoka na mapato yetu kwa kutolipa kodi yetu, ni lazima tubane eneo hilo kama ambavyo sisi tunabanwa tunapokwenda kwao, yeyote aliyeamua kuja kufanya biashara Tanzania ni lazima ajue Tanzania ina sheria zake ikiwemo za ulipaji kodi”
 
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameipongeza TRA kwa kufanikiwa kukusanya Shilingi Trilioni 32.26, sawa na ufanisi wa asilimia 103.9 dhidi ya lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 31.05.
 
“Hii ni hatua ya kihistoria na ya kujivunia kwa kuwa ni mafanikio yanayoakisi dhamira, weledi, na juhudi mlizonazo zinazofanywa na timu ya TRA na uongozi wote katika kuhakikisha mnafikia malengo mliojiwekea”
 
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Wizara ya Fedha kuendelea kufanya maboresho ya Sera, sheria na kuimarisha mifumo ya kodi ili kufikia wigo wa juu wa ukusanyaji kodi bila kuathiri ustawi wa shughuli za kiuchumi.
 
“Kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania, ubunifu mliouonesha mkapata mapato makubwa, endeleeni nao, ubunifu huu umeleta mafanikio makubwa, mbinu rafiki na zakitaalamu mnazotumia kukusanya kodi ziendelezwe, sambamba na kuzingatia Sheria, Utawala Bora, Kanuni na utu”
 
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Wizara hiyo pamoja na TRA wamejipanga kuhakikisha Watanzania wanaelewa kuwa Maendeleo ya nchi yanatokana na kodi.
 
“Wengi wanadhani kuwa fedha za maendeleo zipo Benki Kuu, tunatakiwa kuendelea kuwaelimisha Watanzania kwamba kila kitu cha maendeleo wanachokiona ni fedha zetu, hata fedha za mkopo ni fedha zetu kwa kuwa tutalipa kwa kodi zetu”
 
Naye Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Mwenda amesema kuwa katika mwaka wa fedha ulioishia juni 30, 2025, wameweza kuwarejeshea walipa kodi zaidi ya Shilingi trilioni 1.2 kiwango kikubwa tangu kuanza kwa Mamlaka hiyo “Serikali imerejesha ili kuwezesha biashara zifanye kazi”
 
“Na katika mwaka huu wa fedha tumepanga kukusanya shilingi trilioni 36 ikiwa ni mapato ghafi, tunaamini tukiwa pamoja na walipa kodi tunafanikiwa, tunajua hii ni ndoto ambayo viongozi wetu mnatamani tuitimize”.

No comments:

Post a Comment