Na. Mwandishi wetu, Utete-Rufiji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Mbunge wa Rufiji Mhe. Mohamed Mchengerwa ameungana na wananchi wa Utete Wilayani Rufiji kwenye mazishi ya Bi. Rukia Salum ambaye ni mwananchi wa Utete aliefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Akizungumza na wananchi wa Utete mara baada ya mazishi ya Bi. Rukia Salumu, amewataka waendelee na utamatuni huo wa kushirikiana na kufarijiana ili kuendeleza umoja na mshikamano uliopo miongoni mwao.
Mhe. Mchengerwa amewapongeza wananchi waliojitokeza msibani hapo kuifariji familia ya Bw. Abasi Lijemi na kuwataka kuendeleza utamaduni huo wa kushirikiana na kufarijiana hususani wanapopatwa na misiba.
"Wananchi wenzangu tuendelee kushirikiana na kufarijiana kwani sote tu wapita njia hapa duniani, kikubwa tujiandae ili tukitangulia mbele za haki tupokelewe na Mwenyezi Mungu," Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Aidha, Waziri Mchengerwa ameeleza kuwa marehemu aliugua kwa muda mrefu kidogo na yeye alipata fursa ya kushirikiana familia ya marehemu kugharamia matibabu hospitalini lakini Mwenyezi Mungu amempenda zaidi, hivyo ametoa wito kwa waombolezaji kuendelea kumuombea marehemu ili apokelewe na Mwenyezi Mungu.
Mhe. Mchengerwa ameendeleza utamaduni wake wa kuigusa jamii kwa kushirikiana nayo katika shida na raha jambo ambalo limeendelea kumpa mvuto kwa jamii, ikizingatiwa kuwa yeye ndiye Waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa hivyo anaakisi kwa vitendo kuwa TAMISEMI ni ya WANANCHI na iko kwa ajili ya wananchi kijamii na kimaendeleo.
No comments:
Post a Comment