MWENYEKITI INEC ATOA WITO WA KAMPENI ZA KISTAARABU UCHAGUZI MKUU 2025 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, July 27, 2025

MWENYEKITI INEC ATOA WITO WA KAMPENI ZA KISTAARABU UCHAGUZI MKUU 2025


Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele,Akizungumza jijini Dodoma wakati wa kufungua Mkutano wa Kitaifa kati ya Tume na Vyama vya Siasa kuhusu maandalizi ya uchaguzi 2025.


Na Okuly Julius  OKULY BLOG , DODOMA 


Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele, amevitaka vyama vya siasa kufanya kampeni za kistaarabu zinazoendana na misingi ya amani, sheria na maadili ya kisiasa, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa kufungua Mkutano wa Kitaifa kati ya Tume na Vyama vya Siasa kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo, Jaji Mwambegele alisema kuwa vitendo vya uchochezi na lugha za kashfa vinaweza kuhatarisha utulivu wa nchi na kudhoofisha mchakato wa kidemokrasia.

"Tume inasisitiza umuhimu wa vyama vya siasa kufanya kampeni kwa amani, kwa kuzingatia sheria na kuheshimu wapinzani wao kisiasa. Hili ni jukumu la kila chama na kila mgombea," amesema Mwambegele.

Katika kuhakikisha kuwa vyama vyote 18 vya siasa vinazingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi, Tume imevikabidhi nakala za sheria husika pamoja na maelekezo muhimu yatakayowaongoza katika mchakato mzima wa uchaguzi.

Aidha, Mwenyekiti huyo amebainisha kuwa Tume imekamilisha kazi ya kuainisha idadi ya majimbo ya uchaguzi kwa Tanzania Bara na Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya maandalizi muhimu kuelekea uchaguzi mkuu.

Mhe Mwambegele amesema majimbo yatakayotumika katika uchaguzi kwa Tanzania bara ni 222 huku Zanzibar ni 50.

"Idadi hii ya majimbo ya uchaguzi kuna ongezeko
la majimbo nane (08) yaliyoanzishwa kwa upande wa Tanzania Bara,

"Aidha, jumla ya Kata 3,960 zitafanya uchaguzi wa Madiwani, idadi hii kuna ongezeko la kata tano (05) zilizoongeka baada ya Ofısi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuanzisha kata mpya tano (05)" Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele.

Amesema Tume katika kutekeleza jukumu la kutoa Elimu ya mpigakura, wamejipanga kutoa elimu hiyo kwa njia mbalimbali, imetoa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura kwa taasisi na asasi 164 na kutoa mwaliko kwa taasisi na asasi za ndani na nje ya nchi zenye nia ya kuwa waangalizi wa Uchaguzi kuleta maombi.

"Baada ya mchakato wa uhakiki, jumla ya taasisi na asasi 76 za ndani na 12 za kimataifa zimepata kibali"Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tume, Ramadhani Kailima, ameeleza kuwa maandalizi maalum yanaendelea ili kuhakikisha kuwa mahabusu na wafungwa wanaotimiza vigezo vya kisheria wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi huo.

“Tunajipanga kuhakikisha kuwa haki ya kila Mtanzania, wakiwemo wafungwa na mahabusu, inalindwa. Utaratibu wa kuwahusisha katika upigaji kura uko katika hatua nzuri ya maandalizi,” amesema Kailima.

Mkutano huo wa siku moja unashirikisha viongozi wa vyama vya siasa, maafisa wa uchaguzi na wadau mbalimbali wa demokrasia, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mapema kuelekea uchaguzi mkuu wa kihistoria utakaofanyika mwaka 2025.










No comments:

Post a Comment