SERIKALI YAHIMIZA UTEKELEZAJI WA PROGRAMU YA MALEZI NA MAKUZI YA AWALI YA MTOTO NCHI NZIMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, July 2, 2025

SERIKALI YAHIMIZA UTEKELEZAJI WA PROGRAMU YA MALEZI NA MAKUZI YA AWALI YA MTOTO NCHI NZIMA



Na Okuly Blog, DODOMA


Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Prof. Tumaini Nagu, amewakumbusha na kuwataka Makatibu Tawala wa Mikoa, Maafisa Lishe na Maafisa Maendeleo ya Jamii kuhakikisha wanatekeleza kikamilifu Programu ya Kitaifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (ECDI 2030) ili kuwawezesha watoto wa Tanzania kukua katika mazingira bora na kufikia ndoto zao.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha uwasilishaji wa viashiria vya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kilichofanyika leo jijini Dodoma, Prof. Nagu amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa programu hiyo kuanzia ngazi ya mkoa hadi ngazi ya jamii.

“Ndugu washiriki, natumia fursa hii kuwakumbusha kwenda kutekeleza kikamilifu programu hii ya kitaifa ili kuwawezesha watoto wetu kukua na kufikia utimilifu wao, ndoto zao zitimie na waweze kuwa na mchango mkubwa kwa taifa letu,” alisema Prof. Nagu.

Ameongeza kuwa ni muhimu kwa mikoa na halmashauri zote kutenga bajeti mahsusi kwa ajili ya kuchochea utekelezaji wa programu hiyo katika maeneo yao.

Awali, Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF), Bwana Abbas Mtemba, alieleza kuwa kama taifa bado kuna changamoto kubwa ya kuhakikisha watoto wote wanapata fursa sawa za ukuaji wa kiafya, kielimu, kiakili na kijamii.

“Kama taifa tuna kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha watoto wanakua na kufikia utimilifu unaokusudiwa katika maeneo ya afya, kujifunza, saikolojia na jamii. Tukifanikiwa hapa, tutakuwa tumejenga kizazi chenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi,” alisema Bwana Mtemba.

UNICEF imeahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha mifumo ya utoaji huduma kwa watoto inaimarishwa kwa kiwango bora na stahiki.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (TECDEN), Bi Mwajuma Kibwana, aliwasilisha takwimu za kitaifa zinazoonesha kuwa ni asilimia 47 pekee ya watoto wenye umri wa miezi 24 hadi 59 walio katika hatua ya ukuaji timilifu, huku asilimia 53 wakiwa bado wanakumbwa na changamoto mbalimbali katika malezi na makuzi yao.

“Hali hii ni ya kutia wasiwasi. Tunaiomba Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kuhakikisha wanaboresha hali ya watoto wetu ili kuwa na taifa lenye tija,” alisema Bi Kibwana.

Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makatibu Tawala wa Mikoa kutoka mikoa 15, Maafisa Lishe wa Mikoa na Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka maeneo mbalimbali nchini.






No comments:

Post a Comment