UCHUMI WA WANANCHI WA KAWAIDA WAIMARIKA MARA CHINI YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, July 18, 2025

UCHUMI WA WANANCHI WA KAWAIDA WAIMARIKA MARA CHINI YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA


Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi, akizungumza na Watanzania kupitia mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika mkoa huo leo Julai 18, 2025 katika Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) jijini Dodoma.


Na Okuly Julius, DODOMA


Wananchi wa Mkoa wa Mara wameendelea kunufaika moja kwa moja na utekelezaji wa miradi ya kiuchumi chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Miradi hiyo inajumuisha ujenzi wa masoko ya kisasa, barabara za vijijini, upanuzi wa bandari, pamoja na uwezeshaji wa mitaji kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Akitoa taarifa ya mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, amesema serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika kuboresha maisha ya wananchi wa kawaida kupitia miradi inayochochea uchumi katika ngazi ya kaya na jamii kwa ujumla.

"Katika kipindi hiki, masoko matano ya kisasa yamejengwa katika wilaya za Serengeti (Mugumu), Tarime (Nyamwaga), Butiama (Kwaya), na maeneo mengine. Masoko haya yamewekewa miundombinu muhimu kama maji safi, taa za sola, vizimba vya kufanyia biashara pamoja na vyoo vya kisasa," alisema Kanali Mtambi.

Aidha, amesema kuwa mkoa umetekeleza ujenzi na ukarabati wa barabara zenye jumla ya kilomita 1,137, hatua iliyosaidia kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu na kupunguza gharama za usafirishaji wa mazao kutoka mashambani hadi sokoni.

Kwa upande wa uwezeshaji wananchi kiuchumi, zaidi ya kaya 60,000 kutoka wilaya zote tisa za Mkoa wa Mara zimenufaika na ruzuku kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ambayo imewawezesha kuanzisha miradi ya ufugaji, kilimo cha kisasa na usindikaji wa mazao, na hivyo kuongeza kipato cha familia.

Vilevile, amesema Halmashauri za mkoa huo zimetoa mikopo isiyo na riba yenye thamani ya Shilingi bilioni 4.2 kwa vikundi 1,300 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, jambo lililochochea uanzishaji na ukuaji wa biashara ndogo pamoja na kuongeza ajira kwa makundi hayo maalum.

Kuhusu miundombinu ya biashara, Kanali Mtambi alisema ujenzi unaoendelea wa gati na ghala katika Bandari ya Musoma ni miongoni mwa miradi ya kimkakati itakayosaidia kukuza biashara ya mipakani kati ya Tanzania, Kenya na Uganda kupitia Ziwa Victoria, sambamba na kuongeza mapato ya ndani.

"Mikoa ya pembezoni kama Mara sasa inapata nafasi ya kushiriki kikamilifu kwenye uchumi wa kitaifa kwa kuwa Serikali imejielekeza kuwekeza kwenye miradi ya kimkakati yenye tija kwa wananchi," amesisitiza Mtambi.

No comments:

Post a Comment