
Na. Veronica Mwafisi-Dodoma
Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wamekumbushwa kutanguliza uzalendo wanapotoa huduma kwa wananchi pamoja na kuwa na uelewa mpana wa masuala mbalimbali ya kiutumishi ili waweze kutoa huduma bora kwa maslahi ya Taifa.
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI ambaye ni Naibu Katibu Mkuu, Bw. Xavier Daudi ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa ofisi yake kwenye eneo maalum la mafunzo kwa watumishi wa ofisi hiyo yanayofanyika Mtumba jijini Dodoma kila Jumatatu ya mwanzo wa wiki.
“Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora ina majukumu mengi ikiwemo utoaji wa huduma mbalimbali za kiutumishi hivyo, tutangulize uzalendo na tuhakikishe tunafahamu majukumu yote ya ofisi hii ili tuweze kuwahudumia Watumishi wa Umma na Wananchi kwa maslahi ya Taifa. amesema Bw. Daudi.
Aidha, Bw. Daudi amesisitiza watumishi wa ofisi hiyo kuendelea kuwa waadilifu kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma wanapotekeleza majukumu yao.
Awali akiwasilisha mada kuhusu Maslahi ya Taifa na Ulinzi wa Taifa, Balozi Omar Mjenga amesema, watumishi wa umma wana wajibu wa kuwa wazalendo na nchi yao kwa kuzingatia utii usiokuwa na shaka, kiapo cha utii pamoja na kujitoa kikamilifu kwa maslahi ya Taifa.
Aidha, Balozi Mjenga ameupongeza Uongozi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora pamoja na watumishi wa ofisi hiyo kwa kuwa na utayari wa kuandaa na kushiriki mafunzo kila Jumatatu ya mwanzo wa wiki ili kujenga uelewa kwa watumishi hao kuhusiana na masuala mbalimbali ya kiutumishi.



No comments:
Post a Comment