WAZIRI MKENDA AZINDUA WIKI TATU ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 TEWW - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, July 27, 2025

WAZIRI MKENDA AZINDUA WIKI TATU ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 TEWW



Na Okuly Julius, OKULY BLOG - DODOMA


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali imejidhatiti kuendelea kuimarisha elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi kama chachu ya maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Prof. Mkenda ametangaza rasmi uzinduzi wa wiki tatu za maadhimisho ya miaka 50 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), tangu kuanzishwa kwake mwaka 1975.

"Maadhimisho haya ni fursa ya kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu ya watu wazima katika kukuza maarifa, ujuzi na ustawi wa maisha," amesema Prof. Mkenda.

Maadhimisho hayo yanabeba kauli mbiu isemayo: "Elimu bila ukomo kwa maendeleo endelevu", na yanalenga kuhamasisha ushiriki wa wadau wa kitaifa na kimataifa katika kuendeleza elimu ya watu wazima nchini.

Prof. Mkenda ameeleza kuwa kilele cha maadhimisho hayo kitaadhimishwa kwa kongamano la siku tatu litakalofanyika kuanzia tarehe 25 hadi 27 Agosti, 2025 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, ambapo zaidi ya washiriki 1,000 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kuhudhuria.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa kongamano hilo, huku Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko akifunga rasmi maadhimisho hayo.

Mbali na kongamano hilo, maadhimisho hayo yataambatana na shughuli mbalimbali zikiwemo:

Mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Magereza wanaoendesha programu za kisomo magerezani pamoja na Wakufunzi Wakazi wa TEWW, yatakayofanyika kuanzia Julai 28 hadi 30, 2025 jijini Dodoma.

Maonesho ya elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi, yatakayofanyika katika JNICC kuanzia Agosti 24 hadi 27, 2025, yakihusisha taasisi za umma na binafsi, yakiwa na huduma za ushauri, udahili, na uoneshaji wa bunifu mbalimbali za vijana na watu wazima wanaosomea nje ya mfumo rasmi.

Kongamano la Elimu Bila Ukomo, litakalowakutanisha wataalamu wa elimu ya watu wazima, wakufunzi, watafiti, wanafunzi, viongozi wa serikali, na wawakilishi wa taasisi mbalimbali kujadili mafanikio ya TEWW na mustakabali wa elimu nje ya mfumo rasmi.

Prof. Mkenda ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo ili kujifunza, kupata maarifa mapya, na kuelewa kwa undani mchango wa elimu ya watu wazima katika maendeleo ya Taifa.

"Serikali inaamini kuwa elimu ni haki ya kila mmoja na inapaswa kupatikana bila ukomo, kwa mtu wa rika lolote," amesisitiza Waziri Mkenda.

"Elimu bila ukomo kwa maendeleo endelevu"



No comments:

Post a Comment