
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko Hoza akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Julai 3, 2025, jijini Dodoma, kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika Mkoa huo,

Na Okuly Blog – DODOMA
Zaidi ya shilingi bilioni 196.4 zimetumika kufanikisha miradi ya umeme katika Mkoa wa Katavi katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita, hatua iliyoleta mapinduzi makubwa ya kijamii na kiuchumi katika Mkoa huo ambao awali ulikuwa na changamoto ya upatikanaji wa nishati ya uhakika.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko Hoza, ameeleza hayo Julai 3, 2025, jijini Dodoma wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, akiainisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo sekta za nishati, afya na maji.
Hoza amesema kabla ya kuunganishwa na Gridi ya Taifa, Mkoa wa Katavi ulitegemea vituo vya dizeli vya Mpanda na Mlele, ambavyo havikuweza kukidhi mahitaji.
Amesema hadi kufikia Juni 2025, Mkoa umeunganishwa rasmi na umeme wa Gridi ya Taifa, ambao tayari umewashwa katika Wilaya ya Mlele, Tanganyika na Halmashauri ya Nsimbo.
Mradi huo umegharimu shilingi bilioni 116, ukijumuisha ujenzi wa njia ya msongo wa kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Katavi (km 383) na ujenzi wa vituo vya kupoozea umeme Inyonga (12MW) na Mpanda (28MW).
“Katika kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mkoa wetu umeunganishwa na Gridi ya Taifa, huduma za umeme zimeimarika na vijiji vyote 172 vina umeme kupitia REA,” amesema Hoza.
Aidha, amesema hadi Juni 2025, vitongoji 504 kati ya 912 tayari vimeunganishwa na umeme, huku vilivyobaki 408 vikitarajiwa kufikiwa mwaka wa fedha 2025/2026. Idadi ya wateja imeongezeka kutoka 23,312 mwaka 2021 hadi 42,567 mwaka 2025.
Mapato kutokana na matumizi ya umeme yameongezeka kutoka shilingi milioni 494 kwa mwezi mwaka 2021 hadi zaidi ya bilioni 1 mwaka 2025, huku idadi ya viwanda vikiongezeka kutoka 873 hadi 1,782.
Katika sekta ya afya, Hoza amesema Katavi imetekeleza Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) kwa mafanikio makubwa. Idadi ya vituo vya afya imeongezeka kutoka 102 mwaka 2021 hadi 161 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 36.64.
Zahanati zimeongezeka kutoka 80 hadi 127, vituo vya afya kutoka 17 hadi 28, na hospitali za wilaya nne zimekamilika pamoja na ukarabati wa hospitali ya Manispaa ya Mpanda.
Kwa upande wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Serikali imewekeza shilingi bilioni 18.386 kwa ajili ya miundombinu na vifaa vya kisasa, ikiwa ni pamoja na:
Jengo la huduma za wagonjwa wa nje (OPD),Huduma za akina mama na watoto,ICU, EMD, nyumba ya watumishi, Dialysis, CT-Scan na digital X-Ray.
Amesema mafanikio hayo yamesaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda hospitali za mbali, huku huduma za kibingwa sasa zikitolewa ndani ya Mkoa.
Pia, amesema wastani wa upatikanaji wa dawa umefikia asilimia 94, huku bajeti ya dawa ikiongezeka kutoka bilioni 2.98 mwaka 2021 hadi bilioni 3.38 mwaka 2024. Wajawazito wanaojifungua katika vituo vya afya wameongezeka kutoka 40,269 mwaka 2021 hadi 48,322 mwaka 2025.
Kwa upande wa sekta ya maji, Mhe. Hoza amesema Mkoa wa Katavi umetekeleza miradi mikubwa kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (MUWASA) na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).
MUWASA inatekeleza miradi mitano yenye thamani ya shilingi bilioni 32.16, ikiwemo mradi wa maji wa Milala unaotarajiwa kuzalisha lita milioni 12 za maji kwa siku na kuwahudumia wakazi wote wa Manispaa ya Mpanda. Mradi huu umefikia asilimia 42 na unatarajiwa kukamilika Oktoba 2025.
RUWASA kwa upande wake imetekeleza miradi 51 vijijini kwa thamani ya shilingi bilioni 33.52, ambapo upatikanaji wa maji vijijini umeongezeka kutoka asilimia 62.2 mwaka 2021 hadi 77.3 mwaka 2025.
Mkuu wa Mkoa huyo amesema mafanikio hayo ni ushahidi wa wazi wa dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea Watanzania maendeleo ya kweli.
“Mafanikio haya ni matokeo ya uwekezaji mkubwa wa Serikali katika huduma muhimu za jamii. Katavi leo siyo ile ya jana – tunaendelea kufunguka kimaendeleo na wananchi wananufaika moja kwa moja,” a. Esema Hoza.
No comments:
Post a Comment