
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, amewatunuku vyeti Wafungwa 170 waliomaliza mafunzo ya ujasiriamali na stadi za biashara yaliyotolewa na Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) katika Gereza kuu Arusha.
Hafla ya kutunuku vyeti hivyo ilifanyika tarehe 6 Agosti 2025 katika Gereza Kuu Arusha, ambapo kati ya wahitimu hao, 124 bado wanaendelea kutumikia vifungo vyao gerezani, na 46 wamemaliza kutumikia vifungo vyao.
“Dhamira ya Jeshi la Magereza kuendesha programu hizi ni kuwapa wafungwa ujuzi, kuwawezesha kutekeleza majukumu mbalimbali wakiwa gerezani, na hatimaye kutumia ujuzi huo katika jamii wanapomaliza vifungo vyao,” amesema Bashungwa.
Bashungwa amelielekeza Jeshi la Magereza kuboresha programu za urekebishaji tabia kwa Wafungwa ili kuongeza ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa jamii. Pia amelitaka jeshi hilo kuendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali zitakazowezesha wafungwa kupata mafunzo na ujuzi.
Aidha, Bashungwa amesisitiza umuhimu wa Jeshi la Magereza kuzingatia ujenzi wa miundombinu wezeshi ya sayansi na teknolojia katika ujenzi wa magereza mapya na ukarabati wa magereza ya zamani, ili kuwezesha utoaji wa mafunzo kwa njia ya mtandao kwa ufanisi zaidi.
Awali, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Katungu, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha eneo la urekebishaji tabia kwa wafungwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Modest Mkude, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, amesema Jeshi la Magereza Mkoa wa Arusha limekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza majukumu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utunzaji wa mazingira na upandaji miti.
Nae, Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamini Sedoyeka, amesema mafunzo hayo yalibuniwa kwa kuzingatia uhalisia wa mazingira na mahitaji ya washiriki, hususan katika vipindi vya nadharia na vitendo kwenye fani za uanzishaji biashara, ujasiriamali, vyanzo vya mitaji, usimamizi wa fedha, na utafutaji wa masoko.









No comments:
Post a Comment