
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amesema bunifu za kijasiriamali na teknolojia zinazofanywa na wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) zina mchango mkubwa kwa jamii kwa kuwa zinagusa moja kwa moja mahitaji halisi ya wananchi na kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
RC Sendiga amesema hayo alipotembelea banda la chuo cha Uhasibu Arusha IAA kwenye maonesho ya 31 ya nane nane kanda ya kaskazini yaliyofanyika katika viwanja vya Themi, Njiro -Arusha
Kwa upande wake, Meneja wa Kampasi ya Chuo cha Uhasibu Arusha Dkt. Joseph Daudi amesema chuo kimejipanga kikamilifu kuhakikisha kinatoa elimu bora, yenye kuendana na mahitaji ya soko la ajira kwa kuzingatia ubunifu, teknolojia na ujasiriamali kama nguzo kuu za maendeleo ya kitaaluma
Nae Sarah Adamson, ambaye ni Center Administration Coach wa kituo cha ubunifu na ujasiriamali cha IAA Business Start-Up Center, amesema kupitia mafunzo ya vitendo na ushauri wa kibiashara, kituo hicho kimefanikiwa kulea miradi mbalimbali ya ubunifu ambayo sasa inatoa mchango wa moja kwa moja kwa jamii
“tunajivunia kuona baadhi ya wanafunzi wetu wakigeuza mawazo kuwa biashara halisi, zinazoweza kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla" amesema
Godfrey Chuse mwanafunzi mjasiriamali na mmiliki wa kampuni ya Cabo Group of Companies, inayojishughulisha na Kilimo (shamba direct) pamoja na kutumia mabaki ya mbao kutengeneza mapambano ya nyumbani, amesema kuwa IAA imempa maarifa, ujasiri na jukwaa la kubadilisha ndoto zake kuwa halisi
Chuo cha Uhasibu Arusha kinashiriki katika maonesho ya nane nane yanayofanyika katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Dodoma na Mbeya










No comments:
Post a Comment