DKT. KIRUSWA, SILLO WASHUHUDIA ZOEZI LA UOKOAJI MGODINI SHINYANGA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, August 16, 2025

DKT. KIRUSWA, SILLO WASHUHUDIA ZOEZI LA UOKOAJI MGODINI SHINYANGA



Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, kwa kushirikiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo, wametembelea eneo la tukio la ajali ya mgodi wa Nyandolwa, iliyotokea tarehe 11 Agosti, 2025, katika kijiji cha Mwongozo, Kata ya Mwenge, Halmashauri ya Shinyanga, kushuhudia juhudi zinazoendelea za uokoaji wa mafundi waliokwama chini ya ardhi baada ya kuangukiwa na kifusi.

Ajali hiyo ilitokea kwenye eneo lenye leseni ya uchimbaji inayomilikiwa na kikundi cha wachimbaji wadogo maarufu kama Wachapakazi, ambapo mafundi wapatao 25 walikuwa wakifanya kazi ya ukarabati katika mashimo matatu tofauti ya uchimbaji dhahabu.

Katika ziara hiyo, Dkt. Kiruswa ametoa salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao pamoja na salamu za pole kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Mheshimiwa Rais Samia amenituma rasmi kufikisha salamu zake za pole kwa waathirika wote wa ajali hii. Amesikitishwa sana na tukio hili na anafuatilia kwa karibu hatua zote za uokoaji,” amesema Dkt. Kiruswa.

Kwa upande wake, Mhe. Sillo ameeleza kuwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linafanya kazi kwa bidii kuhakikisha kuwa mafundi waliokwama wanapatikana haraka. Amesisitiza umuhimu wa kuzingatia taratibu za usalama migodini, na kutoa wito kwa wamiliki wa migodi kote nchini kuhakikisha mazingira salama kwa wafanyakazi wao.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Julius Mtatiro, ambaye pia yupo katika eneo la tukio, ametoa ufafanuzi kuhusu hali ya uokoaji na idadi ya mafundi waliokuwa katika kila duara wakati ajali ilipotokea.

Taarifa ya Maendeleo ya Uokoaji Mtatiro ameeleza kuwa hadi kufikia tarehe 16 Agosti, mafundi watano wameokolewa, huku mafundi wengine 20 wakiendelea kutafutwa.

Amesema katika hao watano waliookolewa, mmoja alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu hospitalini na mwingine alikutwa tayari amefariki dunia ndani ya moja ya mashimo.

Mgawanyo wa mafundi kwa kila duara ni kama ifuatavyo:
Katika hatua nyingine, Mtatiro ameeleza mgawanyo wa mafundi kwenye kila duara, amesema, duara namba 106 lenye urefu wa mita 40 Mafundi 6 walikuwa kazini, wanne wameokolewa, mmoja kati yao alifariki akiwa anapatiwa matibabu katika Kituo cha Afya cha Salawe na watatu wako hai.

Amesema duara namba 103 lenye urefu wa mita 130 Mafundi 11 walikuwa kazini, mmoja amekutwa amefariki dunia, juhudi za kuwatafuta wengine zinaendelea na duara namba 20 ambalo lina urefu wa mita 75, mafundi 8 walikuwa kazini, juhudi za uokoaji bado zinaendelea.

“Tuendelee kupambana hadi tuhakikishe tunawatoa watu wetu salama. Rais ametoa maagizo mahsusi ambayo yameanza kutekelezwa kwa asilimia kubwa, ikiwemo kuongezwa kwa nguvu kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,” ameeleza Mtatiro.

Ameongeza kuwa zoezi la uokoaji linafanyika kwa ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za serikali, Kampuni ya Barrick Bulyanhulu, wataalamu wa sekta ya madini, na wananchi wanaoendelea kujitolea kusaidia.

Katika tukio hilo lenye mvutano wa kihisia na changamoto nyingi, matumaini bado yako hai huku timu ya uokoaji ikiendelea na kazi usiku na mchana kwa kutumia vifaa maalum vya kisasa na msaada wa kitaalamu.

Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kuimarisha usimamizi wa usalama migodini, hususan kwa wachimbaji wadogo, ili kuhakikisha matukio kama haya hayajirudii tena. Familia za waathirika pia zitaendelea kupatiwa msaada wa karibu na huduma muhimu mgodi hapo.




No comments:

Post a Comment