MAABARA YA KISASA GEITA KUWAINUA WACHIMBAJI KANDA YA ZIWA – MAVUNDE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, August 21, 2025

MAABARA YA KISASA GEITA KUWAINUA WACHIMBAJI KANDA YA ZIWA – MAVUNDE



Na Mwandishi Wetu, Geita.


Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Peter Mavunde, amesema ujenzi wa maabara ya kisasa ya utafiti na uchambuzi wa madini katika mkoa wa Geita ni hatua kubwa itakayosaidia kuwainua wachimbaji wa madini Kanda ya Ziwa na kuimarisha mchango wa Sekta ya Madini katika uchumi wa taifa.

Akizungumza leo Agosti 21, 2025 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa maabara hiyo, Mhe. Mavunde amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kukubali ombi la Wizara la kujenga maabara tatu za kisasa nchini.

Amesema mbali na maabara hiyo inayojengwa Geita itakayogharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.5, maabara nyingine itajengwa Chunya mkoani Mbeya na maabara kubwa zaidi kimataifa itajengwa jijini Dodoma.

“Maabara hizi zitakuwa nguzo ya utafiti wa kisayansi wa sampuli za madini, kuongeza ufanisi wa wachimbaji wadogo na kupunguza gharama na usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizi, zitakuwa na vifaa vya kisasa zaidi” amesema Mavunde.

Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ndiyo moyo wa shughuli za madini hapa nchini kupitia kazi ya utafiti wa kijiolojia, hivyo kuanzishwa kwa kituo hicho kutasaidia kuchochea shughuli za madini hususan katika Ukanda wa Ziwa ambao unaongoza kwa shughuli za uchimbaji hapa nchini, zikiwemo mikoa ya kimadini ya Geita, Mbogwe, Kagera, Mwanza, Kahama, Mara na Shinyanga.

“Kwa mwaka uliopita pekee, sekta ya madini ilikusanya maduhuli shilingi bilioni 328 kutoka Mkoa wa Kimadini ya Geita, jambo linaloonesha mchango mkubwa wa ukanda huu katika pato la taifa na ndiyo maana uwekezaji huo umefanywa na Serikali hapa” amesisitiza Mavunde.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella, amesisitiza kuwa maabara hiyo itapunguza muda na gharama kwa wananchi waliokuwa wakilazimika kusafiri hadi Dodoma kufuata huduma hizo.

“Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia kwa kuona umuhimu wa kutuletea kituo hiki muhimu. Ni msaada mkubwa kwa wachimbaji na wananchi wetu wa Kanda ya Ziwa,” amesema RC Shigella.

Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Maabara wa GST, Notika Bandeze, amesema maabara hiyo1 mpya itakuwa na vifaa na mitambo ya kisasa zaidi, ikiwemo ya utambuzi wa madini, uchunguzi wa sampuli, pamoja na utoaji wa taarifa za kina za kijiolojia zinazohitajika na wachimbaji na wawekezaji.

Ujenzi wa maabara ya madini Mkoani Geita unatarajiwa kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali, kuokoa muda na mitaji kwa wachimbaji, na kuimarisha mchango wa sekta ya madini katika maendeleo ya taifa.






No comments:

Post a Comment