Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya habari kusini mwa Afrika,Tawi la Tanzania (MISA TAN) Bw. Edwin Soko, akizungumza mwanzo mwa kikao kazi baina ya taasisi hiyo na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwenye jengo la kitegauchumi la Mfuko huo, PSSSF Commercial Complex jijini Dar es Salaam, Agosti 14, 2025
Meneja Mafao Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Bw. Ramadhan Mkeyenge, akitoa mada kuhusu shughuli za Mfuko, kwenye kikao kazi baina ya PSSSF na Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika -MISA-TAN (Tawi la Tanzania) kwenye ukumbiw a jengo la PSSSF Commercial Complex jijini Dar es Salaam Agosti 14, 2025.
Meneja Uwekezaji PSSSF, Bw. Herman Goodluck.
Baadhi ya washiriki wa kikao kazi baina ya PSSSF na Taasisi ya Vyombo vya habari kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TAN), wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zikiwasilishwa na wataalamu ya Mfuko
Wajumbe wakizungumza kwenye kikao hicho
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA-TAN), Bw. Edwin Soko, ameupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), kwa kuendelea kutoa huduma nzuri kwa wanachama ikiwemo kulipa pensheni ya mwezi kwa wakati na kuendesha majukumu yake kwa uwazi.
Bw. Soko ameyasema hayo jijini Dar es Salaam Agosti 14, 2025 kwenye kikao kazi baina ya waandishi wa habari ambao ni wanachama wa MISA na PSSSF ili kueleza mafanikio ya utekelezaji wa majukumu ya Mfuko.
“ Naipongeza sana PSSSF kwa kuamua kukutana na waandishi hawa ambao ni wanachama wa MISA bila ya uoga wowote, taasisi yoyote safi inakubali kukutana na waandishi wa habari. Hatua yenu ya kukutana na sisi mmetuheshimisha, ninyi hambagui waandishi wa habari,” alisema Bw. Soko.
Akizungumzia huduma za PSSSF, mshiriki wa kikao hicho kutoka Zanzibar, Bw. Othman Maalim, ameipongeza PSSSF kwa uboreshaji wa huduma zake na kutoa ushuhuda wake wa kupokea mafao ndani ya muda mfupi baada ya kustaafu utumishi wa umma katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki.
“Natoa pongezi kwa PSSSF kwa huduma bora na ningependa kutoa wito muendelee hivyo na kwa wengine, unapostaafu unakwenda kupambana na maisha ya nje ya kazi hivyo unahitaji msukumo wa haraka wa kupata Mafao,” alisema Bw. Maalim.
Mstaafu mwingine kutoka Sumbawanga na aliyewahi kuwa mtangazaji wa Radio Tanzania Dar es Salaam (TBC), Bw. Nswima Ernest, yeye alisema ulipaji wa pensheni kwa wastaafu umeboreshwa.
“Wakati watumishi wa umma mishahara yao inalipwa tarehe 25 ya kila mwezi, kwa sisi wastaafu kuanzia tarehe 21 ya kila mwezi mwisho 24 lazima pesa itakuwa imeingia kwenye Akaunti yako ya benki, mafao kwa sisi si tatizo tena yanakuja kwa wakati,” alisema Bw. Ernest.
Akizungumzia mafanikio ya utekelezaji wa majukumu ya Mfuko, Meneja wa Mafao PSSSF, Bw. Ramadhan Mkeyenge, alisema mafanikio hayo yametokana na maboresho katika utoaji wa huduma kwa kuongeza matumizi ya TEHAMA ikiwemo kuwawezsha wanachama kupata huduma kupitia simu janja.
“Utoaji wa huduma kupitia mtandao umerahisisha utekelezaji wa majukumu ya mfuko kama vile kusajili wanachama, kuwasilisha madai ya Mafao mbalimbali, lakini pia hata ulipaji wa Mafao,” alisema.
Akizungumza katika kikao hicho, naye Meneja Uwekezaji PSSSF, Bw. Herman Goodluck, amesema asilimia 60% ya uwekezaji wa Mfuko uko kwenye Hati Fungani za Serikali ambako usalama ni mkubwa, huku asilimia nyingine zilizobaki zimewekezwa kwenye majengo na taasisi za kifedha ikiwa ni pamoja na kuingia ubia na kampuni zingine ili kulinda na kuongeza thamani ya Mfuko.
No comments:
Post a Comment