MKOA WA DODOMA WAZINDUA MKAKATI MAALUM WA KUTANGAZA VIVUTIO VYA UTALII - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, August 21, 2025

MKOA WA DODOMA WAZINDUA MKAKATI MAALUM WA KUTANGAZA VIVUTIO VYA UTALII



Na Gideon Gregory, Dodoma


Katika jitihada za kuhakikisha sekta ya utalii nchini inaendelea kuimarika, Mkoa wa Dodoma umezindua mkakati maalum wa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika mkoa huo.

Kupitia mkakati huo, Serikali ya Mkoa inalenga kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi kwa kuvitangaza vivutio mbalimbali, ikiwemo maeneo ya kihistoria, tamaduni za wenyeji pamoja na mandhari ya kipekee yanayopatikana Dodoma.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika leo Agosti 21,2025 hapa Jijini Dodoma, Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha ajenda ya mkakati wa Utalii inasimamiwa na kuwa endelevu.

"Kadhalika na bodi ya utalii endeleeni kuchagiza jinsi gani ya kufanya na kuratibu masuala ya utalii na hasa kuyafunganisha Mkoa wa Dodoma na maeneo mengine, lengo kubwa ni kwamba eneo hili liwe habu ya utalii kama malengo ya Mkuu wa Mkoa na wenzake walivyokusudia katika maeneo haya,"amesema.

Pia, ameitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI yenye kazi ya kupanga mipango miji kushirikiana na Wizara ya Ardhi wahainishe maeneo maalum ya kujenga shughuli za utalii zenye kuvutia suala zima la kujenga utalii.

Aidha, Waziri Dkt. Jafo amewaomba wananchi kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha wanachagiza katika upande huo wa utalii.

"Sisi wenyeji wa Dodoma kwanza wakarimu, ukitaka watu wakarimu njoo Dodoma utawakuta, tutumue ukarimu wetu kuhakikisha ajenda hii ya utalii inasonga mbele kwa maslahi mapana ya Tanzania lakini halikadhalika na mkoa wetu wa Dodoma,"ameomba.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema mkakati huo utakuwa muongozo wa kuonyesha na kutambulisha aina zote za utalii ndani ya mkoa huo pamoja na ukuzaji wa uchumi.

"Leo ni siku ya kihistoria kwa sekta ya utalii wa Mkoa wa Dodoma, kwani wanazindua mkakati ambao si tu utaimarisha taswira ya Dodoma kimataifa kama kivutio cha utalii bali pia utachochea ukuaji wa uchumi, uboreshaji wa ajira na maendeleo ya jamii ya mkoa kwa ujumla, "anasema.

Ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika jitihada zake za kuendeleza na kukuza sekta ya utalii nchi imeendelea kuandaa mazingira rafiki ya uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta hiyo ya utalii.

Mkurugenzi Msaidizi wa Utalii kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Richie Wandwi ametoa wito kwa mikoa mingine nchini kufuata nyayo za mkoa wa Dodoma katika kuzindua mikakati kama hiyo inayolenga kukuza utalii endelevu na unao wajibika.

"Tunapoongelea uendelezaji wa shughuli za utalii tunagusa mengi, tuna mazao mbalimbali ya utalii, lakini uendelezaji huu hauwezi kufanyika kiholela kwahiyo tunapokuwa na nyenzo kama hizi za kimkakati tunaenda kuhakikisha kabisa kama nchi, kama mkoa wetu wa Dodoma tunakuwa na utalii ambao unapiga hatua zaidi,"amesema.

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Dodoma Pendolake Elinisafi amesema kupitia mkakati huo wataenda kuongeza matokeo chanya katika ukusanyaji wa kodi.

"Mkakati wa kukuza utalii si tu unachangia kuongeza pato la taifa bali pia unaimarisha misingi ya mapato ya ndani kupitia kodi na kama tunavyofahamu dhamira ya Serikali ya sasa ni kuimarisha makusanyo ya ndani na kupunguza utegemezi kutoka nchi wahisani,"amesema.









No comments:

Post a Comment