
Benki ya NMB imekabidhi hundi ya zaidi ya shilingi bilioni 1.9 kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, kwa ajili ya mikopo ya vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu kupitia mpango wa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Makabidhiano hayo yalifanyika jana katika hafla ya uzinduzi wa utoaji wa mikopo hiyo, ambapo Mkuu wa Mkoa Senyamule alisisitiza umuhimu wa benki kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa kwa wakati, ili kuendeleza jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuwezesha makundi maalum kiuchumi.
“Kupitia mikopo hii, wananchi watekeleze miradi yenye tija na kuhakikisha wanarejesha kwa wakati ili na wengine waweze kunufaika. Mikopo hii si zawadi, ni mkopo nafuu usio na riba, hivyo ni wajibu wa kila mnufaika kuitumia vyema,” alisema Senyamule.
Katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa pia alikabidhi mikopo ya pikipiki kwa kikundi cha Bodaboda cha Kituo cha Magufuli kilichopo Mji wa Serikali Mtumba, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango huo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dkt. Fredrick Sagamiko, jumla ya shilingi bilioni 3.6 zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya vikundi 308 kupitia Halmashauri ya Jiji la Dodoma, fedha ambazo zimekusanywa kutokana na mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kipindi cha miaka miwili.









No comments:
Post a Comment