SERIKALI YALIPA FIDIA YA SHILINGI MILIONI 999 KWA WANANCHI 103 WA DODOMA KWA MIRADI YA MAJI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, August 13, 2025

SERIKALI YALIPA FIDIA YA SHILINGI MILIONI 999 KWA WANANCHI 103 WA DODOMA KWA MIRADI YA MAJI


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Maji, imekamilisha zoezi la ulipaji wa fidia yenye jumla ya Shilingi Milioni 999 kwa wananchi 103 ambao ardhi yao ilitwaliwa katika maeneo ya Nzuguni, Zuzu Nala, Nala Chihoni na Kibaigwa kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maji inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA).

Ulipaji wa fidia hizo, umeongozwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DUWASA, Wizara ya Ardhi na Viongozi wa Serikali za Mitaa wa maeneo husika, ambapo kwa eneo la Nzuguni, Wananchi 24 wamelipwa fidia ya Shilingi Milioni 148 tarehe 07 Agosti, 2025, Zuzu Nala Wananchi 51 ambao wamelipwa fidia ya Shilingi Milioni 594 Agosti 11, 2025, Nala Chihoni Wananchi 7 ambao walilipwa fidia yao ya Shilingi Milioni 58 tangu mwezi Aprili, 2025 na Kanda ya Kibaigwa Wananchi 23 wamelipwa fidia ya Shilingi Milioni 197 na kukamilisha zoezi hilo Agosti 12, 2025.

Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa kiasi hicho cha fedha kwa wananchi waliyotoa ardhi yao kupisha utekelezaji wa miradi ya maji.

"DUWASA, kwa niaba ya Wananchi wa maeneo ya Nzuguni, Zuzu Nala, Nala Chihoni na Kibaigwa, inaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita na Wizara ya Maji kwa juhudi zao kubwa na ufanisi katika kuhakikisha ulipaji wa fidia kwa wakati kwa wananchi wetu," alisema Mhandisi Aron.

"Hatua hii ni muhimu sana kwa maeneo yaliyotekelezwa na yanayoendelea na utekelezaji wa miradi ya maji ya kimkakati katika Jiji la Dodoma na Kanda ya Kibaigwa, hii inaonesha dhamira ya Serikali katika kulinda haki za wananchi wakati wa kutekeleza miradi ya maendeleo." Amesma Mhandisi Aron.

Kwa upande wa wakazi wa Kibaigwa, Bi. Josephina Paulo ameishukuru serikali kwa kuwasikiliza na kuwalipa fidia. Ameiomba serikali kwa kuwaona wanyonge na kuwafikia wengine ambao bado hawajalipwa wanasubiri kulipwa.

Naye Bwa. Yohana Mwarabu ameshukuru serikali kwa kumjali na kumlipa kwani sasa ataenda kujenga nyumba nyingine ili aweze kuishi na familia yake kwani awali hakuwa na matumaini lakini kwa sasa anaamani.

Fidia hiyo ni sehemu ya maandalizi ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa na Serikali kupitia DUWASA iliyokusudiwa kuboresha upatikanaji wa majisafi na huduma za usafi wa mazingira ka wakazi wa jiji la Dodoma na maeneo mengine yanayohudumiwa na DUWASA.

No comments:

Post a Comment