
Serikali ya Singapore na Tanzania zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo na kiuchumi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo uendeshaji wa bandari, utalii, sekta ya fedha, usafirishaji, biashara na uwekezaji, elimu na kilimo ili kuchochea kasi ya maendeleo ya Taifa na wananchi wake.
Makubaliano hayo ambayo yatatekelezwa kupitia Programu ya Ushirikiano wa Singapore (Singapore Cooperation Program), yamefikiwa wakati wa mazungumzo yaliyofanyika terehe 28 Agosti 2025, kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Singapore Mhe. Dkt.Vivian Balakrishnan jijini Singapore.
Katika hatua ya awali ya utekelezaji wa makubaliano hayo Tanzania na Singapore zimeazimia kukamilisha na kutia saini Mkataba wa Kulinda Uwekezaji wa Kutotoza Kodi mara mbili ikiwa ni hatua muhimu za kuvutia uwekezaji na biashara kati ya nchi hizo mbili.
"Singapore na Tanzania zote zipo katika maeneo la kijiografia ambayo ni lango la biashara na uwekezaji. Hivyo ushirikiano wa nchi zetu mbili unaweza kufungua masoko ya nchi zaidi ya 30 za Afrika na Asia" Alieleza Waziri Balakrishnan.
Kwa upande wake, Waziri Kombo alieleza kuwa, Serikali ya Tanzania itaendelea kuweka mazingira salama na rafiki kwa biashara na uwekezaji huku akisisitiza kuhusu umuhimu wa kuongeza ushirikiano katika sekta zinazogusa maisha ya wananchi ya kila siku ikiwemo maji, nishati, nyumba na makazi, bidhaa za chakula, sekta ya fedha, elimu na uzalishaji wa bidhaa za kiteknolojia.
Vilevile katika mazungumzo hayo Waziri Balakrishnan ameahidi kuongeza wigo wa fursa za ufadhili wa elimu na mafunzo kwa watanzania hususan vijana, katika nyanja mbalimbali ikiwemo teknolojia na ubunifu ili kuwaongezea uwezo utakao wawezesha kumudu ushindani wa soko la ajira na kujiajiri.
Aidha, Waziri Balakrishnan amaebainisha kuwa kupitia Programu ya Ushirikiano wa Singapore, serikali ya nchi hiyo itaongeza wigo wa fursa za ufadhili wa elimu na masomo kwa vijana wa Tanzania ili kuwajengea uwezo wa kumudu ushindani wa soko la ajira na kujiajiri.
Aliendelea kufafanua kuwa mkakati huo utajumuisha mafunzo ya muda mrefu na mfupi, mafunzo ya ufundi, pamoja na programu za ubadilishanaji wa uzoefu ambao utawawezesha vijana wa kitanzania kupata ujuzi na maarifa ya kisasa ya kuendesha sekta za kimkakati ikiwemo uchumi wa kidijitali, usimamizi wa miradi, nishati mbadala na ujasiriamali.
Katika kipindi cha miongo miwili ya hivi karibuni Tanzania imesajli wawekezaji 32 kutoka nchini Singapore wakiwa na uwekezaji wenye thamani zaidi ya Dola za Marekani milioni 500 huku wakitoa ajira kwa zaidi ya watu 3000.



No comments:
Post a Comment