Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson (Mb), ametangaza kwa masikitiko makubwa kifo cha Spika Mstaafu na aliyewahi kuwa Mbunge wa Kongwa, Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, kilichotokea leo jijini Dodoma.
Katika taarifa rasmi kwa umma iliyotolewa na Ofisi ya Bunge, Spika Dkt. Tulia amesema:
“Kwa masikitiko makubwa, naomba kutoa taarifa ya kifo cha kiongozi wetu, mwanasiasa mkongwe na Spika Mstaafu wa Bunge Mheshimiwa Job Yustino Ndugai kilichotokea leo jijini Dodoma. Natoa pole kwa familia ya Marehemu, ndugu, jamaa na Wananchi wa Jimbo la Kongwa. Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu,” amesema Mheshimiwa Spika.
Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Kamati ya Mazishi pamoja na familia ya marehemu imeanza maandalizi ya mazishi, na taarifa zaidi kuhusu mipango hiyo zitatolewa kadri zitakavyokamilika.
Marehemu Job Yustino Ndugai alizaliwa tarehe 22 Januari 1963 na amefariki dunia tarehe 6 Agosti 2025, akiacha historia ndefu ya utumishi wa umma, hususan katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment