TANZANIA YACHAGULIWA KUWA MWENYEJI FEASSA 2026. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, August 25, 2025

TANZANIA YACHAGULIWA KUWA MWENYEJI FEASSA 2026.



Tanzania imechaguliwa kwa mara ya tano kuwa mwenyeji wa mashindano ya michezo ya wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari kwa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEASSA) kwa mwaka 2026.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Michezo Ofisi ya Rais – TAMISEMI Bw. George Mbijima, Tanzania imepata fursa hiyo kufuatia mzunguko wa uandaaji wa michezo hiyo ambayo inafanyika kila mwaka katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Bw. Mbijima amesema hayo wakati akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa Tanzania walioshiriki mashindano ya michezo ya FEASSA 2025, Kakamega nchini Kenya alipokuwa akiwaaga katika kambi ya michezo katika Chuo cha Ualimu Tarime mkoani Mara kabla ya kurudi katika shule zao kuendelea na masomo.

Aidha, amesema kutokana na fursa ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo kwa mwaka 2026, Tanzania inakusudia kuwa na washiriki zaidi ya 1,000 ili kuongeza wigo wa kushinda na kutoa fursa zaidi kwa wanamichezo wa Tanzania kupata uzoefu wa kushiriki katika michezo ya kimataifa.

“Lengo siyo kuongeza wingi wa washiriki, ila tunahitaji wanamichezo wetu wapate uzoefu zaidi na tunahitaji medali na vikombe vingi ili kuieshimisha nchi yetu kama mwenyeji na kulitangaza jina la Tanzania ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu" alisema Bw. Mbijima.

Awali Mratibu wa Michezo kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Yusuph Singo alisema wanamichezo pamoja na walimu wote waliokwenda kushiriki mashindano ya michezo ya FEASSA nchini Kenya wamerejea salama.

Mara ya mwisho Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya FEASSA ilikuwa mwaka 2022, ambapo yalifanyika Jijini Arusha, yakiwashirikisha zaidi ya wanafunzi 900 kutoka nchi za Afrika Mashariki.




No comments:

Post a Comment