Kongwa, Dodoma
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia mradi wa Uboreshaji Barabara za Vijijini kwa Ushirikishaji wa Jamii na Ufunguaji wa Fursa za Kijamii na Kiuchumi (RISE) umeendelea kutoa mafunzo ya matengenezo madogo madogo ya barabara kwa vikundi 24 katika Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.
Mafunzo hayo yanalenga kuwapatia vikundi hivyo fursa na elimu ya umuhimu wa wananchi kushiriki moja kwa moja kwenye matengenezo na maboresho ya kazi mbalimbali kupitia programu ya CBRM (Community Based Road Maintenance).
Programu inayowapatia wananchi fursa ya kushiriki kazi ndogo ndogo kama vile kusafisha mitaro, kusafisha hifadhi ya barabara, kufyeka majani kwa kutumia vifaa vya kawaida kama majembe na mafyekeo.
Aidha, Mhandisi Faizer Mbange ametoa elimu zaidi juu ya vifaa mbalimbali vitakavyotumika katika kazi za matengenezo pamoja na umuhimu wa kuzingatia usalama, matumizi ya alama na vifaa vya usalama mahali pa kazi.
Vilevile, Afisa Ustawi wa Jamii, Bi. Joha Rashid amesisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki katika matengenezo na kuwa walinzi na wahamasishaji kwa wananchi wengine pia kutunza miundombinu hiyo.
No comments:
Post a Comment