NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Suleiman Serera, akizungumza wakati wa Warsha ya Kitaifa ya Utetezi na Uenezi wa Muhtasari wa Sera za Usalama wa Chakula kwa Watoa Maamuzi wa Ngazi ya Juu iliyofanyika leo, Agosti 14, 2025 jijini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu – Dodoma
NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Suleiman Serera, ametoa wito kwa sekta zote nchini kuingiza masuala ya usalama wa chakula katika sera na mipango yao, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa kulinda afya ya wananchi na kukuza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na ya kimataifa.
Akizungumza jijini Dodoma leo, Agosti 14, 2025, wakati wa Warsha ya Kitaifa ya Uenezi wa Muhtasari wa Sera za Usalama wa Chakula kwa Watoa Maamuzi wa Ngazi ya Juu, Dk. Serera amesema usalama wa chakula si jukumu la sekta moja pekee, bali linahitaji ushirikiano mpana kati ya serikali, sekta binafsi na jamii kwa ujumla.
“Usalama wa chakula si suala la kiufundi pekee – ni nguvu ya umma, pasipoti ya ushindani wa kibiashara, na msingi wa ukuaji wa viwanda,” amesema Dk. Serera. “Kama msemo wa Kiswahili unavyosema: chakula salama ni afya, afya ni maisha na maisha ni maendeleo.”
Aidha,Dk. Serera,amezitaka mamlaka za serikali za mitaa kupewa uwezo zaidi wa kudhibiti viwango vya chakula katika masoko rasmi na yasiyo rasmi. Pia amesisitiza umuhimu wa kusaidia wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs) katika kuhakikisha matumizi ya viungio salama vya chakula, kuweka lebo sahihi, na kudumisha usafi katika mnyororo mzima wa thamani wa bidhaa za chakula.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) alizozitoa, zaidi ya watu milioni 91 barani Afrika huugua kila mwaka kutokana na ulaji wa chakula kisicho salama, huku watu takribani 137,000 wakipoteza maisha. Hali hiyo husababisha hasara kubwa za kiuchumi kutokana na kupungua kwa uzalishaji na kupotea kwa fursa za kibiashara.
Hata hivyo Dk. Serera amesisitiza kuwa Tanzania haiwezi kufanikisha ndoto ya kuwa “kapu la kuzalisha chakula salama Afrika” bila kuwekeza kwa kina katika usalama wa chakula. Ametoa wito kwa serikali, sekta binafsi, taasisi za elimu, na washirika wa maendeleo kushirikiana kwa karibu katika kufanikisha dhamira hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dk. Ashura Katunzi, amesema kuwa shirika hilo linaendelea na juhudi za kuhamasisha utekelezaji wa muhtasari wa sera nne muhimu zinazolenga kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Dk. Katunzi ameeleza kuwa sera hizo zimebuniwa kushughulikia changamoto mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa chakula, kutoka hatua ya uzalishaji hadi kwa mlaji.
“Sera hizo zinajumuisha udhibiti wa mabaki ya viuatilifu kwenye mazao ya kilimo na mifugo, uchafuzi wa chakula, pamoja na kuhakikisha usalama katika mnyororo mzima wa thamani wa chakula – kuanzia shambani hadi mezani,” amesema Dk. Katunzi.
Aidha amebainisha kuwa utekelezaji madhubuti wa sera hizo utaongeza ulinzi kwa mlaji, kuboresha afya ya jamii, na kuongeza ushindani wa bidhaa za chakula za Tanzania katika soko la kimataifa.
Naye Mratibu wa Miradi kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Diomedes Kalisa, amesema kuwa shirika hilo kwa kushirikiana na WHO linaendelea kuisaidia Tanzania kuandaa viwango vya chakula salama vinavyokidhi matakwa ya kimataifa.
Aidha amebainisha kuwa hatua hiyo itaiwezesha Tanzania kupanua biashara za chakula kupitia mikataba ya kikanda na kimataifa kama vile AfCFTA, EAC, SADC na WTO-SPS.

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Suleiman Serera, akizungumza wakati wa Warsha ya Kitaifa ya Utetezi na Uenezi wa Muhtasari wa Sera za Usalama wa Chakula kwa Watoa Maamuzi wa Ngazi ya Juu iliyofanyika leo, Agosti 14, 2025 jijini Dodoma.

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Suleiman Serera, akizungumza wakati wa Warsha ya Kitaifa ya Utetezi na Uenezi wa Muhtasari wa Sera za Usalama wa Chakula kwa Watoa Maamuzi wa Ngazi ya Juu iliyofanyika leo, Agosti 14, 2025 jijini Dodoma.

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dk. Ashura Katunzi,akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Warsha ya Kitaifa ya Utetezi na Uenezi wa Muhtasari wa Sera za Usalama wa Chakula kwa Watoa Maamuzi wa Ngazi ya Juu iliyofanyika leo, Agosti 14, 2025 jijini Dodoma.

MRATIBU wa Miradi kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Diomedes Kalisa,akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Warsha ya Kitaifa ya Utetezi na Uenezi wa Muhtasari wa Sera za Usalama wa Chakula kwa Watoa Maamuzi wa Ngazi ya Juu iliyofanyika leo, Agosti 14, 2025 jijini Dodoma.

SEHEMU ya washiriki wakifuatilia mada mbalimbali wakati wa Warsha ya Kitaifa ya Utetezi na Uenezi wa Muhtasari wa Sera za Usalama wa Chakula kwa Watoa Maamuzi wa Ngazi ya Juu iliyofanyika leo, Agosti 14, 2025 jijini Dodoma.

SEHEMU ya washiriki wakisikiliza hotuba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Suleiman Serera (hayupo pichani) wakati wa Warsha ya Kitaifa ya Utetezi na Uenezi wa Muhtasari wa Sera za Usalama wa Chakula kwa Watoa Maamuzi wa Ngazi ya Juu iliyofanyika leo, Agosti 14, 2025 jijini Dodoma.

SEHEMU ya washiriki wakifuatilia mada mbalimbali wakati wa Warsha ya Kitaifa ya Utetezi na Uenezi wa Muhtasari wa Sera za Usalama wa Chakula kwa Watoa Maamuzi wa Ngazi ya Juu iliyofanyika leo, Agosti 14, 2025 jijini Dodoma.

SEHEMU ya washiriki wakifuatilia mada mbalimbali wakati wa Warsha ya Kitaifa ya Utetezi na Uenezi wa Muhtasari wa Sera za Usalama wa Chakula kwa Watoa Maamuzi wa Ngazi ya Juu iliyofanyika leo, Agosti 14, 2025 jijini Dodoma.

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Suleiman Serera,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua Warsha ya Kitaifa ya Utetezi na Uenezi wa Muhtasari wa Sera za Usalama wa Chakula kwa Watoa Maamuzi wa Ngazi ya Juu iliyofanyika leo, Agosti 14, 2025 jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment