
Na Okuly Julius, OKULY BLOG – Dodoma
Mbinu ya RIFLEKTI inayochanganya ufundishaji wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) sambamba na stadi za maisha kama ujasiriamali, kilimo bora na ufugaji wa kisasa, ndiyo imekuwa kiini cha mafunzo ya siku tatu yaliyotolewa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kwa wawezeshaji wa madarasa ya Kisomo kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Kupitia mbinu hiyo, washiriki walijengewa uwezo wa kutumia vielelezo shirikishi (PRA tools) kuwasaidia wanafunzi kutambua changamoto zinazowakabili katika jamii zao, kupanga mipango kazi, na kuzitatua kwa vitendo kwa kutumia maarifa ya KKK na stadi za maisha.

Mafunzo hayo, yaliyofanyika kuanzia Julai 28 hadi 30, 2025, yaliwaleta pamoja washiriki 32 wakiwemo maafisa 20 kutoka magereza ya Isanga (Dodoma), Iringa, Lindi, Ruanda (Mbeya) na Butimba (Mwanza), pamoja na wakufunzi wakazi 6 na wawezeshaji wa madarasa ya Kisomo kutoka mikoa ya Katavi, Rukwa, Simiyu, Dar es Salaam, Dodoma na Tabora.
Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo, Dkt. Enedy Mlaki, Mkufunzi Mkazi wa TEWW – Dodoma, kwa niaba ya Mkuu wa Taasisi hiyo Prof. Philipo Sanga, amesema mbinu ya RIFLEKTI imekuwa chachu ya mafanikio katika Elimu ya Watu Wazima kwa sababu inaweka msukumo wa maarifa katika maisha halisi ya wanafunzi.
“Mbinu hii ya RIFLEKTI siyo tu inawapa watu stadi za msingi za KKK, bali pia inawawezesha kupata ujuzi wa moja kwa moja wa shughuli za kiuchumi, hivyo kuchangia ustawi wao wa kijamii na kiuchumi,” amesema Dkt. Mlaki.
Aidha, washiriki walielimishwa juu ya saikolojia ya mtu mzima, mbinu bora za kujifunzia na kufundishia, pamoja na matumizi sahihi ya zana za kufundishia katika madarasa ya Kisomo. Walikabidhiwa pia Miongozo ya Wawezeshaji inayowasaidia kupanga, kutekeleza na kutathmini masomo kwa kuzingatia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023), inayosisitiza mafunzo ya amali.
Dkt. Mlaki ameeleza kuwa Elimu ya Watu Wazima ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya Taifa kwa kuwa inawapa watu wazima na vijana waliokosa fursa ya elimu rasmi nafasi ya kupata stadi za kujitegemea, kama vile useremala, ushonaji na ujenzi.
Kwa mujibu wa takwimu, takriban asilimia 17 ya Watanzania wazima bado hawana stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu. Hali hiyo inaifanya TEWW kuendelea kubuni na kutekeleza programu madhubuti kama MUKEJA ili kupunguza kiwango hicho na kusaidia taifa kufikia maendeleo endelevu.







No comments:
Post a Comment