WMA YAWAONDOA HOFU WAKULIMA WA PAMBA KUHUSU UHALALI VIPIMO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, August 6, 2025

WMA YAWAONDOA HOFU WAKULIMA WA PAMBA KUHUSU UHALALI VIPIMO


Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo mkoa wa Simiyu, Bi. Happy Titi, akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 06,2025 katika Banda la WMA kwenye Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.


Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Wakala wa Vipimo (WMA) imewatoa hofu wakulima wa pamba kuhusu uhalali na usahihi wa vipimo vinavyotumika katika ununuzi wa zao hilo, ikisisitiza kuwa vipimo hivyo ni sahihi na vinafuatiliwa kwa ukaribu ili kuwalinda walaji na wazalishaji dhidi ya udanganyifu.

Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo mkoa wa Simiyu, Bi. Happy Titi, amesema hayo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Banda la WMA kwenye Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

“Lengo kubwa la Wakala wa Vipimo ni kumlinda mlaji katika sekta ya afya, biashara, nishati na nyinginezo,” amesema Bi. Happy Titi.

Ameeleza kuwa katika maonesho hayo, WMA inatoa elimu kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wadau wengine wa sekta mbalimbali ili kuwawezesha kuelewa umuhimu wa kutumia vipimo sahihi katika shughuli zao.

Akizungumzia sekta ya kilimo, Bi. Titi amesema kuwa elimu hutolewa kuanzia hatua za awali za maandalizi ya mashamba, ambapo maafisa kilimo hushirikiana na WMA kuhakikisha vipimo vinavyotumika ni sahihi na vimehakikiwa kabla ya matumizi.

“Kipimo chochote kabla hakijaanza kutumika ni lazima kipimwe. Wakaguzi wetu wanaendelea na ufuatiliaji kuhakikisha hakuna anayevunja sheria kwa kuchakachua vipimo. Wale watakaobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua ikiwemo kutozwa faini au kufikishwa mahakamani,” amesisitiza.

Kwa mujibu wa Bi. Titi, WMA itaendelea kushirikiana na wadau wote ili kuhakikisha vipimo vinavyotumika katika sekta zote vinazingatia viwango vya kitaifa na kimataifa kwa manufaa ya wananchi.








No comments:

Post a Comment